Kaulimbiu ya siku ya mwaka huu ni “Hatua za miji kukabiliana na changamoto”na Umoja wa Mataifa unasema miongoni mwa changamoto hizo ni migogoro, mabadiliko ya tabianchi, na ukosefu wa utulivu wa kisiasa ambazo zimewalazimisha watu milioni 123 duniani kote kuyahama makazi yao  wengi wakisaka usalama katika miji iambayo tayari imeelemewa huku huduma za afya, maji, na makazi zikifikia ukomo.

Katika ujumbe wake wa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “Takribani mtu mmoja kati ya wanane anaishi katika makazi duni, na zaidi ya watu milioni 300 hawana nyumba kabisa kote duniani.”

Murrombua, Msumbiji. UN-Habitat imetekeleza miradi ya kuboresha usalama wa makazi na ustahimilivu, kupunguza uwezekano wa jamii za ndani kukumbwa na vimbunga na majanga mengine.

UN Habitat

Murrombua, Msumbiji. UN-Habitat imetekeleza miradi ya kuboresha usalama wa makazi na ustahimilivu, kupunguza uwezekano wa jamii za ndani kukumbwa na vimbunga na majanga mengine.

Lakini ameongeza kuwa suluhisho halipo tu kwenye majengo, bali kwenye ujumuishwaji.

Amesema “Miji si mawe na matofali pekee. Ni ahadi ya kuwa na nyumbani. Tujenge pamoja miji imara inayohakikisha usalama na ujumuishwaji kwa wote.”

Kamishna Mkuu wa Wakimbizi Filippo Grandi anasisitiza ujumbe huo akisema miji ndiyo inakuwa mstari wa mbele kwa watu waliokimbia makazi yao duniani kote.

Anasema “Leo, zaidi ya asilimia 60 ya watu milioni 123 waliolazimika kuyahama makazi yao wanaishi mijini. Ufurushwaji huu kimsingi ni changamoto ya makazi.”

Kuanzia Sudan hadi Ukraine, na kutoka Syria hadi Afghanistan Grandi anasema urejeshaji wa miji na uwekezaji katika nyumba za gharama nafuu lazima uende sanjari na misaada ya kibinadamu.

Akiongeza kuwa “Misaada ya kibinadamu pekee haitoshi. Suluhisho lazima liendane na mipango ya maendeleo ya kitaifa na mikakati ya ujenzi mpya katika ngazi za kitaifa.”

Hata hivyo amesema kuna dalili za matumaini katika nchi kama Kenya, Ethiopia, na Mauritania ambako kambi za wakimbizi zinabadilika na kuwa jamii za mijini zilizojumuishwa.

Amesisitiza kuwa “Ukweli ni kwamba  ufurushwaji wa watu tayari unabadilisha sura ya miji yetu. Kuimarisha uwezo wa miji kukabiliana na changamoto na kujumuisha watu waliolazimika kuhama ni moja ya changamoto kubwa zaidi tulizo nazo na ni fursa tunayopaswa kuitumia.”

Katika Siku hii ya Makazi Duniani, ujumbe wa Umoja wa Mataifa uko bayana, miji si hifadhi tu dhidi ya migogoro, bali ni injini za ujumuishaji na mnepo kwa dunia inayosonga mbele.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *