
Shirika la hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limefanikisha uhamishaji wa tembo takribani 500 kutoka katika maeneo ya wananchi na mwekezaji wilayani Kyerwa na Karagwe kuelekea Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato.
Zoezi hilo endelevu, ambalo linatekelezwa kitaalamu kwa ushirikiano kati ya TANAPA na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), lilihusisha uhamishwaji wa makundi makubwa mawili yenye tembo zaidi ya mia 100, waliotembea umbali wa zaidi ya kilometa 150 kutoka Kyerwa kuelekea ndani ya Hifadhi ya Taifa Burigi – Chato.
Zoezi hilo, linakuja baada ya wataalamu wa Ikolojia kutoka shirika hilo kuyafuatilia makundi hayo kwa ukaribu zaidi.
“Zoezi linaendelea vizuri licha ya changamoto kadhaa zinazojitokeza kwa tembo wakorofi ambao hujitenga na wenzao, pia endeleeni kuyafuatilia yale makundi ambayo mmeshayafikisha hifadhini ili yasirudi tena na kwenda kusababisha karaha kwa wananchi na mali zao japo kwa umbali waliotembea na misukosuko waliyoipata ni vigumu kurudi, ila tuendelee kuwachunguza kwa ukaribu,” alisema Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara wa TANAPA, Massana Mwishawa.