Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia Maria Zakharova amesema, kuna ushahidi mpya unaoonyesha kuwa Ukraine inayasaidia makundi ya wanamgambo na ya kigaidi katika eneo la Sahara-Sahel barani Afrika, ikiwa ni pamoja na kuyasambazia ndege zisizo na rubani,

Akizungumza katika mkutano na wanahabari, Zakaharova ameeleza kwamba, Kiev inatoa wakufunzi na ndege zisizo na rubani kusaidia “operesheni za kigaidi” katika nchi za Niger na Sudan.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameashiria taarifa zilizohusishwa na Kanali Fat-h al-Sayid wa Idara ya Intelijensia ya jeshi la Sudan ambaye amesema, mamluki wa Ukraine na Colombia wanapigana bega kwa bega na wanamgambo wa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) wa nchini Sudan ikiwa ni pamoja na kutumia ndege zisizo na rubani zilizotengenezwa Ukraine.

Kwa mujibu wa Zakharova, harakati za makundi ya kigaidi katika nchi kadhaa za Afrika zimehusishwa na uuzaji haramu wa silaha zilizotolewa na nchi za Magharibi kwa Ukraine.

“Silaha kama hizo zimeripotiwa kupatikana miongoni mwa makundi ya kigaidi nchini Burkina Faso, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mali, Niger, Sudan, Somalia, Syria, Jamhuri ya Afrika ya Kati, na Chad,” ameeleza msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Russia.

Mnamo mwezi Juni, afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan aliiambia chaneli ya Russia Today kwamba Kiev ilikuwa inalipatia silaha kundi la wanamgambo la RSF. Alisema, Ukraine ilikuwa ikifanya “kazi chafu” ya nchi za Magharibi kwa kuunga mkono makundi yanayobeba silaha yanayohusika na mashambulizi ya kigaidi katika nchi za Libya, Somalia na Niger.

Mwezi uliopita, Waziri Mkuu wa Mali, Abdoulaye Maiga aliishutumu Ukraine kwa kusambaza ndege zisizo na rubani za Kamikaze kwa makundi ya kigaidi na kuonya kwamba utoaji silaha unaofanywa na nchi za Magharibi kwa Kiev unaweza kuchochea ugaidi duniani. Mali ilivunja uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine mnamo Agosti 2024, ikinukuu taarifa za maafisa wa Ukraine waliodai kuhusika na kusaidia makundi ya wabeba silaha yaliyohusika katika shambulio la 2024 huko Tinzaouaten…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *