
Mashindano ya mbio za nusu marathoni za Lake Victoria (Lake Victoria Half Marathon 2025) yamefanyika juzi Jumapili huku Kampuni ya Mawasiliano ya Simu za mkononi, YAS kwa kushirikiana na huduma za kifedha za kidijitali Mixx, imejitosa kuungana na wadau mbalimbali wa michezo katika kuunga mkono jitihada za kusaidia watoto njiti kama sehemu ya kuchangia maendeleo ya jamii.
Akizungumza jijini Mwanza baada ya kumalizika kwa mbio hizo, Kaimu Mkurugenzi wa YAS Kanda ya Ziwa, Robert Sanyagi alisema mbio hizo hazikulenga tu ushindani wa riadha, bali zilikuwa na dhamira pana zaidi ya kusaidia watoto njiti katika Hospitali za Rufaa za Sekou Toure na Bugando, ambao huhitaji uangalizi maalumu ili waweze kukua na kufanikisha ndoto zao.
“Takwimu zinaonyesha zaidi ya watoto 120 huzaliwa njiti kila mwezi katika hospitali hizi mbili. Kupitia mbio hizi, tumechangia kutoa matumaini mapya kwa familia zinazopitia changamoto za gharama za matibabu na kuokoa maisha ya vizazi vijavyo,” alisema Sanyagi.
Sanyagi alibainisha mbio hizo zimekuwa kichocheo cha uchumi wa Jiji la Mwanza, zikileta manufaa kwa mama lishe, wauzaji wa vinywaji, madereva wa magari ya usafirishaji, hoteli, pamoja na wafanyabiashara wa vifaa vya michezo na matangazo.
“Hii ni ithibati kwamba michezo si burudani tu, bali ni injini muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” alisema Sanyagi aliyefafanu kwa upande wa teknolojia kuwa YAS na Mixx zitaendelea kutumia ubunifu na huduma zake za kidijitali kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
“Mtandao wetu wa 4G na 5G umewezesha wananchi wa Kanda ya Ziwa kuunganishwa kwa urahisi zaidi, huku huduma za kifedha kama Lipa kwa Simu zikirahisisha biashara kufanyika kidijitali. Tunaamini michezo na teknolojia vina nguvu ya kushirikiana, michezo ikijenga afya na umoja, teknolojia ikirahisisha mawasiliano na fursa,” alisema.
Mratibu wa Mbio za Lake Victoria Half Marathon, Hilda Vigo, alitoa shukrani kwa mchango mkubwa katika kufanikisha mbio hizo, akisema ushirikiano wa sekta binafsi ni nguzo muhimu katika kukuza michezo nchini.
“Tunashukuru sana YAS na Mixx kwa kuwa sehemu ya safari hii ya mabadiliko. Mchango umekuwa chachu kubwa katika kufanikisha malengo ya kusaidia watoto njiti na kukuza uchumi wa Mwanza kupitia michezo. Tunatarajia ushirikiano huu utaendelea kwa miaka mingi ijayo,” alisema Vigo.
Mbio za Lake Victoria Half Marathon zimeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha jamii, wadau wa michezo, na sekta binafsi katika kuunga mkono maendeleo endelevu kupitia michezo na matendo ya kijamii.