“Tunampongeza María Corina Machado kwa kutangazwa mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel,” amesema msemaji wa OHCHR, Thameen Al-Kheetan . “Heshima hii inaonesha matarajio ya wazi ya watu wa Venezuela ya kuwa na uchaguzi huru na wa haki, haki za kiraia na kisiasa, na utawala wa sheria. Kamishna Mkuu ameendelea kusimama imara akitetea maadili haya.”

Mwanaharakati huyo mwenye umri wa miaka 58, ambaye alizuiwa kugombea katika uchaguzi wa urais mwaka jana, anaishi mafichoni ndani ya Venezuela na alikamatwa kwa muda mfupi baada ya kuhudhuria mkutano wa upinzani mwezi Januari. Aliachiliwa haraka, ikiripotiwa kuwa ni kutokana na shinikizo la kimataifa.

Bi. Machado apokea kwa unyenyekevu

Bi. Machado ameshukuru Kamati ya Nobel kwa heshima hiyo akisema “ni mafanikio ya jamii nzima… Mimi ni mtu mmoja tu. Kwa kweli sistahili hii tuzo.”

Ushahidi thabiti wa kuwepo kwa vizuizi vikubwa dhidi ya uhuru wa kiraia nchini Venezuela umetajwa katika ripoti nyingi zilizoagizwa na Baraza la Haki za Binadamu. Mapema mwaka huu, wachunguzi huru wa haki za binadamu waliotoa ripoti kwa Baraza hilo mjini Geneva walihimiza mamlaka za Venezuela kusitisha tabia ya kuwatia kizuizini wapinzani wa kisiasa bila mawasiliano.

Walisema kwamba “ukamatwaji huu unaolenga makundi maalum” ni kinyume cha sheria na unalingana na kutoweshwa kwa kulazimishwa, ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu iwapo utathibitishwa, na huenda ukawa ni uhalifu wa kimataifa.

Ukiukaji haki wafurutu ada Venezuela

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Volker Türk, pia amekuwa akielezea wasiwasi wake mara kwa mara kuhusu madai ya ukiukaji wa haki katika taifa hilo la Amerika Kusini.

Mwezi Desemba 2024, Bwana Türk alisisitiza kuhusu “matumizi ya nguvu kupita kiasi na vurugu” wakati wa maandamano baada ya uchaguzi mapema mwaka huo, “ikiwemo na watu wenye silaha wanaounga mkono serikali,” ambayo yalisababisha vifo vya watu wasiopungua 28.

Mwezi Julai, Bunge la Kitaifa la Venezuela lilimtangaza Bwana Türk pamoja na wafanyakazi wa OHCHR kuwa watu wasiotakiwa nchini humo, hatua iliyozuia kazi za haki za binadamu za UN nchini humo.

Tunataka kuendeleza ushirikiano

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Bwana Al-Kheetan amesisitiza kuwa OHCHR inataka kuendelea kushirikiana na serikali ya Venezuela na wadau wengine wote. “Tunasalia na dhamira thabiti ya kuendelea kutetea na kulinda haki za binadamu za wavenezuela wote, iwe wako ndani ya Venezuela au nje ya nchi, tukizingatia taarifa na kuweka waathirika katika kiini cha kazi yetu,” amesema.

“Jambo la msingi hapa ni kwamba tunahitaji ushirikiano zaidi na mamlaka; kama mnavyojua, Bunge la Kitaifa la Venezuela lilipiga kura kuunga mkono kumtangaza Kamishna Mkuu kuwa mtu asiyetakiwa nchini  humo na hili ni jambo tunalolijutia sana.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *