Ripoti mpya ya WHO iliyopewa jina “Kuokoa maisha, kutumia gharama ndogo” iliyotolewa leo sanjari na maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Dunini , inaonesha kuwa uwekezaji wa ziada wa dola 3 tu kwa kila mtu kwa mwaka unaweza kuokoa maisha ya watu milioni 12 na kuleta faida za kiuchumi zinazofikia zaidi ya Dola trilioni 1 ifikapo mwaka 2030.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema  “Magonjwa yasiyo ya kuambukiza na matatizo ya afya ya akili ni wauaji wa kimyakimya, wanaotunyima maisha na ubunifu. Kuwekeza katika mapambano dhidi ya NCDs si tu uchumi bora ni hatua ya haraka na muhimu kwa ustawi wa jamii.”

Maendeleo yamepungua licha ya hatua za awali

Kwa mujibu wa tathmini mpya ya WHO, nchi 82 zimepunguza vifo vinavyotokana na NCDs kati ya mwaka 2010 na 2019, lakini kasi ya maendeleo imepungua sana. Asilimia 60 ya mataifa yalishuhudia kusimama au kurudi nyuma kwa mafanikio, hasa katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati ambazo tayari ndizo zinazoathirika zaidi.

Ripoti inasema Denmark imeongoza kwa mafanikio makubwa zaidi, huku China, Misri, Nigeria, Urusi na Brazil pia zikionesha kupungua kwa vifo vinavyosababishwa na NCDs.

Hata hivyo, ongezeko la vifo vinavyotokana na saratani ya kongosho, ini na magonjwa ya mishipa au neva limepunguza mafanikio hayo.

Nchi maskini zinabeba mzigo mkubwa zaidi

NCDs ikiwemo magonjwa ya moyo, saratani, magonjwa sugu ya mfumo wa kupumua na kisukari ndiyo yanayosababisha vifo vingi duniani imesema ripoti hiyo.

Imeongeza kuwa watu zaidi ya bilioni moja wanaishi na matatizo ya afya ya akili, na karibu robo tatu ya vifo vinavyohusiana na hali hizi hutokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.

WHO inakadiria kuwa watu milioni 32 hupoteza maisha kila mwaka katika maeneo hayo.

“Hivi ni vifo vinavyoweza kuzuilika,” amesisitiza Dkt. Tedros. “Tuna zana zilizothibitishwa kuokoa maisha, lakini mataifa mengi yanashindwa kuzitumia ipasavyo.”

Suluhu zipo na ni nafuu

Ripoti hiyo ya WHO inasisitiza kuwa suluhu za kupambana na NCDs na kukuza afya ya akili zipo na zinagharimu kidogo.

Utekelezaji wa hatua za “Best Buys” za WHO kama vile kodi kwa bidhaa za tumbaku na pombe, kudhibiti shinikizo la damu, na kuongeza uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi unahitaji dola chache tu kwa kila mtu kwa mwaka.

“Ni jambo lisilokubalika kwamba maslahi ya kibiashara yanaendelea kunufaika kutokana na vifo na magonjwa yanayoongezeka,” amesema Dkt. Etienne Krug, Mkurugenzi wa Idara ya WHO inayoshughulika na Vihatarishi vya Afya, Uhamasishaji na Kuzuia Magonjwa.

Ameongeza kuwa “Serikali lazima ziweke watu mbele ya faida na kuhakikisha sera za afya zinazotegemea ushahidi haziingiliwi na shinikizo za kibiashara.”

Mwingilio wa makampuni unazuia sera za kuokoa maisha

WHO imeonya kuwa makampuni yenye nguvu ikiwemo yale ya tumbaku, pombe na vyakula vilivyosindikwa kupita kiasi yanaendelea kushawishi dhidi ya sera ambazo zingesaidia kuokoa maisha. Hatua hizo za ushawishi, shirika linasema, zinadhoofisha jitihada za serikali kuweka kodi za afya, kudhibiti matangazo, na kuwalinda watoto dhidi ya masoko hatarishi.

“Makampuni haya yana nguvu na fedha nyingi,” ameongeza Dkt. Krug. “Lakini hakuna faida inayopaswa kuwekwa juu ya afya ya umma.”

Ari ya kisiasa yahitajika kabla ya mkutano wa UN

Katika mkutano wa nne wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu NCDs na afya ya akili HLM4, uliofanyika tarehe 25 Septemba huko New York, WHO imezitaka nchi wanachama kutumia fursa hiyo kupitisha tamko thabiti la kisiasa litakalohakikisha uwekezaji na uwajibikaji upya.

“Tunajua nini kinafanya kazi. Wakati wa kuchukua hatua ni sasa,” alisema Dkt. Devora Kestel, Mkurugenzi wa Idara ya WHO kwa NCDs na Afya ya Akili. “Serikali zitakazochukua hatua kwa uthabiti zitaokoa maisha, kupunguza gharama na kukuza uchumi. Watakaochelewa watalipa kwa kupoteza maisha na uchumi dhaifu.”

Fursa ya kihistoria kwa kizazi hiki

WHO inatoa wito wa ongezeko la fedha za ndani, kuimarishwa kwa huduma za afya ya msingi, upatikanaji mpana zaidi wa dawa muhimu, na mifumo imara ya uwajibikaji.

Shirika hilo linasema mkutano wa HLM4 ni fursa muhimu zaidi ya muongo huu ya “kubadili ahadi kuwa matendo.”

“Ulimwengu wenye afya bora na usawa zaidi uko mikononi mwetu,” amesema Dkt. Tedros. “Tunachohitaji sasa ni ujasiri, uongozi na uwekezaji ili kufanya hili liwe halisi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *