Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) jana Ijumaa lilitoa wito wa kutekelezwa juhudi za kimataifa haraka iwezekanavyo ili kukabiliana na mgogoro unaoongezeka wa wakimbizi katika eneo la Sahel barani Afrika, ambapo takriban watu milioni 4 wamelazimika kuhama makazi yao huko Burkina Faso, Mali, Niger na katika nchi nyingine jirani.

Abdouraouf Gnon-Konde Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika wa Kuhudumia Wakimizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) katika eneo la Magharibi na Katikati mwa Afrika amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kwamba eneo la Sahel barani Afrika haliwezi kukabiliana na changamoto zote hizi pekee yake. 

Ametahadharisha kuwa hali ya mchafukoge, uhaba wa chakula na athari za hali ya hewa zinapelekea idadi kubwa ya watu kuhama makazi yao. 

Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika wa Kuhudumia Wakimizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) katika eneo la Magharibi na Katikati mwa Afrika ameeleza kuwa wanawake na watoto wanaunda asilimia 80 ya waliokimbia makazi yao, huku unyanyasaji wa kijinsia na uandikishwaji wa kulazimishwa ukiongezeka. Zaidi ya shule 14,800 na vituo vya afya 900 vimefungwa hivi sasa.

Shirika la UNHCR limeeleza kuwa hadi sasa limepokea asimilia 32 tu ya fedha ilizoahidhiwa kutoka kwa wafadhili. Konde amehimiza kuchukuliwa hatua za pamoja na endelevu kimataifa ili kuwalinda mamilioni ya watu na kurejesha matumaini katika eneo la Sahel barani Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *