Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza Bongo Fleva imeshuhudia video rasmi ya muziki iliyotengenezwa kwa teknolojia ya akili unde (Artificial Intelligence – AI), nayo ni ya wimbo wake Nandy, Sweety (2025) ambao ameshirikiana na Jux.
Video hiyo ambayo imetengenezwa na AI9ja Studios kwa gharama ya Dola4,500, wastani wa Sh11 milioni, imetoka hivi karibuni na ndani ya siku moja ilitazamwa zaidi ya mara milioni 1.3 katika mtandao wa YouTube.
Hata hivyo, mafanikio hayo ya kiteknolojia yanazidi kuibua maoni mseto miongoni mwa mashabiki na wadau na sio Bongo tu bali duniani kote.
Wapo wanaosema ni lazima muziki ubadilike kuendana na ukuaji wa teknolojia, pia wapo wenye mashaka kuhusu hatma za ajira kwa waongozaji wa video za muziki.
Akili Unde (AI) ni teknolojia inayowezesha mashine au kompyuta kufikiri, kujifunza, kufanya maamuzi na hata kutenda kama binadamu, kwa kutumia maarifa na uzoefu wake bila kuhitaji msaada.
Sasa katika video hiyo, mastaa hao wanaonekana kukutana katika mitaa ya Hollywood, Los Angeles nchini Marekani. Jux anamuomba namba ya simu Nandy, ambaye anatoa kiroho safi tu kisha kila mmoja anashika njia yake.
Jux anapofika nyumbani kwake, anachukua simu na kumpigia Nandy, wanazungumza kwa bashasha kubwa na hatimaye wanakubaliana wakutane katika mgahawa kwa ajili ya kupata kinywaji pamoja.
Kila moja anavaa na kupendeza vilivyo, wanapokutana wanakunywa na kisha kuondoka pamoja ndani ya gari usiku huo.
Siku inayofuata jioni yake, wanaenda kucheza pamoja ufukweni na kuchora mapenzi yao juu mchanga, wakimaanisha kuwa upendo wa kweli ndio umetawala kati yao.
Siku chache mbele, Billnass ambaye ni mume wa Nandy, anapokea simu kutoka kwa rafiki yake Jux ambaye anamwambia atazame katika simu yake kwani amemtumia picha za mpenzi wake mpya.
Upande wa pili, Nandy anachati na rafiki yake, Priscilla ambaye ni mke wa Jux. Nandy anamueleza kuwa wiki iliyopita alikutana na jamaa mmoja na wakapendana sana. Priscilla anasema tuma picha nimuone shemeji!.
Ghafla picha inayotumwa ni ya mumewe Jux, kule napo Billnass anashangaa kutumiwa picha ya mkewe Nandy!.
Kumbe Jux na Nandy hawakuelezana ukweli kwamba wote wana ndoa zao, na kibaya zaidi nao walikuwa hawajui kuwa rafiki zao wana ndoa zao pia.
Akizungumzia mradi huo, Nandy amesema baada ya kutoa video ya awali (visualizer) ya wimbo huo na ikafanya vizuri, aliona kuna sababu ya kuja na kitu cha tofauti ambacho kitaonyesha ubunifu.
“Nikasema tutarudi na video gani ambayo itafanya tuonekane tumefanya kitu cha maana au video itakayomfanya mtu apate stori ya kuingolea. Nikafikiria mimi na Jux tuigize uhalisi ni kitu hakiwezekani, sisi ni wanandoa lazima tuheshimu ndoa,” amesema.
“Kutokana na nafuatilia vitu, nikasema AI ni kitu kizuri sana kama tukipata mtu ambaye atafanya katika ubora na stori ikawa nzuri. Nikafikiri itakuwa ni kitu kizuri na sisi tutakuwa watu wa kwanza kufanya hivyo, nikapelekwa wazo wakalipinga,” ameeleza Nandy.
Hata hivyo, baada ya majadiliano ya wiki takribani mbili pamoja na kuwashirikisha baadhi ya waongozaji wa video, Nandy na Jux walikuja kukubaliana kufanya tu video ya AI.
Lakini hatua hii ya wasanii kutumia akili unde (AI) katika kutengeneza video za nyimbo zao inaweza kuathiri vipi ajira za waongozaji video?.
“Uhalisi utabakia kuwa uhalisia, wale sio watu wa kweli, yale ni makatuni,” anafafanua Nandy na kuongeza.
“Waongozaji waelewe ikitokea kuna dharura na sababu za kufanya hivyo ipo, tumeshaletewa urahisi wa kufanya hivyo. Lakini kushuti katika uhalisi kama una wazo zuri, bado kuna haja kuendelea kufanya hivyo,” Nandy ameeleza.
Ikumbukwe wimbo huo wa Nandy, Sweety (20250, ni wimbo wenye mahadhi ya Afro Pop unaozungumzia mapenzi kwa njia ya kipekee kwa kuchanganya lugha tatu.
Lugha hizo ni Kiswahili, Kiingereza na Naija ambayo imeleta neno kama ‘Joro’ katika ngoma hiyo, likiwa na maana ya mpenzi.
Ukiwa umeimbwa kwa sauti laini na mtiririko wa kuvutia masikioni kwa wengi, wimbo huu (Sweety), unabaki kuwa matokeo ya upendo wa dhati na furaha ya kuwa katika hali ya kupendana.
Nandy, mwanzilishi wa chapa ya The African Princess, hii ni mara ya kwanza kushirikiana na Jux, mwanachama wa zamani wa kundi la Wakacha lilotamba na ngoma kama Here We Go (2011) na Facebook Girl (2011).