Katibu Mkuu wa shirika la kijeshi la NATO Mark Rutte amesema, nchi kadhaa wanachama wa shirika hilo zitachangia kwa pamoja shehena ya silaha na zana za kijeshi yenye thamani ya yuro milioni 400 kwa ajili ya Ukraine, ambazo zitanunuliwa kutoka Marekani.

Kwa mujibu wa Rutte, Denmark, Estonia, Finland, Iceland, Latvia, Lithuania, Norway na Sweden zinatarajiwa kufadhili kifurushi hicho kupitia mpango wa Orodha ya Mahitaji ya Ukraine Iliyopewa Kipaumbele. Mpango huo uliidhinishwa mnamo mwezi Septemba, na kuiruhusu Marekani iipatie silaha Kiev ambapo gharama za silaha hizo zitalipwa na wanachama wa Ulaya wa NATO.

Rais wa Marekani, Donald Trump, amekuwa mara kwa mara akimkosoa mtangulizi wake Joe Biden kwa kutoa vifurushi vikubwa vya misaada ya kijeshi kwa Ukraine na kumuelezea rais wa nchi hiyo Vladimir Zelensky kama “muuzaji mkubwa zaidi duniani.” Pia amesisitiza kwamba wanachama wa NATO barani Ulaya wanabeba mzigo mkuu wa kuiunga mkono Ukraine.

Mapema wiki hii, rais huyo wa Marekani alidai tena kwamba Washington imetumia dola bilioni 350 katika mzozo wa Ukraine na kwamba serikali yake haitatenga tena fedha hizo. 

Trump amezungumzia jinsi Washington inavyorejesha gharaa zake kwa kusema: “sasa wao wanatulipa kupitia NATO”.

Tangazo hilo linatolewa huku Kiev ikizidi kuandamwa na uchunguzi wa ufisadi ambao umeongeza mashinikizo kwa serikali ya Zelensky.

Mapema wiki hii, Ofisi ya Taifa ya Kupambana na Rushwa ya Ukraine iliwashtaki watu saba, akiwemo mshirika wa zamani wa kibiashara wa Zelensky, Timur Mindich, kwa kuhusika na rushwa na ubadhirifu katika sekta ya nishati, ambayo inafadhiliwa kwa kiasi kikubwa na misaada ya Magharibi. Mwanadiplomasia mkuu wa EU, Kaja Kallas, ameitaka Kiev kushughulikia ufisadi “haraka sana” akisisitiza kwamba “pesa za wananchi inapasa ziende mstari wa mbele (wa vita).”

Russia kwa upande wake, imekuwa ikiwashutumu waungaji mkono wa Ulaya wa Ukraine kwa kurefusha muda wa mzozo na vita baina ya nchi hizo mbili kwa gharama ya maisha ya Waukreni, ikisema, nchi hizo haziko tayari kukiri kwamba mkakati wao umefeli na kugonga mwamba…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *