Russia na China ambazo ni wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimetaka kufutwa kikamilifu “Tume ya Amani” kwenye matini ya rasimu iliyowasilishwa na Marekani kwenye baraza kuhusu Gaza.

Russia na China Ijumaa, tarehe 14 Novemba,  zilipinga rasmi toleo lililorekebishwa la rasimu ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Gaza. Rasimu hiyo ambayo iliwasilishwa na Marekani ilitayarishwa kwa mujibu wa mpango wa vipengee 20 wa Donald Trump kwa ajii ya kusitisha vita na kuijenga upya Gaza  na imejikita kuhakikisha kuwa kikosi cha kimataifa cha askari jeshi kitatumwa katika eneo hilo la Palestina hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2027.

Rasimu hiyo iliyofanyiwa marekebisho ilichapishwa Alhamisi iliyopita ambapo sasa imejumuisha mabadiliko madogo. Hata hivyo rasimu hiyo ingali inasisitiza kuundwa Tume ya Amani ya muda kwa ajili ya kuisimamia masuala ya Gaza. Tume hiyo inatazamiwa kuwa na jukumu la kukisimamia kikosi cha askari jeshi wa kulinda amani na suala upokonyaji silaha  kikamilifu katika Ukanda wa Gaza, kutoa mafunzo kwa jeshi la polisi la Palestina, kusimamia mipaka kati ya Misri na utawala wa Israel na kuwezesha misaada ya kibinadamu.

Mauaji ya kimbari ya Israel na Marekani dhidi ya Gaza 

Russia na China, nchi wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa ambazo zina haki ya kura ya veto, zimetaka kufutwa kikamilifu “Tume hiyo ya Amani” katika matini rasimu ya azimio. Wanadiplomasia wa nchi mbili hizo wamesema kuwa, zaidi ya nusu ya matini hiyo ya rasimu iliyopendekezwa haitoshi, haiko wazi au haijajumuisha masuala ya dharura, na kusisitiza kuwa kikosi cha askari jeshi wa kulinda amani kinapaswa kuwajibika kwa kusimamiwa  moja kwa moja na Baraza la Usalama na si tume fulani ya muda ambayo inaweza kuwa chini ya ushawishi wa Marekani na Israel.

Nchi hizo mbili zinasisitiza kuwa upo ulazima kwa Umoja wa Mataifa kusimamia kikamilifu kikosi chochote cha kigeni huko Gaza na zinaamini kuwa rasimu hiyo haitoshi kuwadhaminia Wapalestina haki zao, na kwamba haionyeshi njia ya wazi ya kuelekea kuundwa taifa huru la Palestina. Russia na China zimesema zitapiga kura ya turufu dhidi ya rasimu hiyo iwapo haitafanyiwa mabadiliko ya kimsingi.

Sababu za upinzani wa Russia na China:

1. Wasiwasi kuhusu ushawishi wa Marekani na Israel 

Azimio hilo lililopendekezwa na Marekani linajumuisha kuanzishwa kile kilichopewa jina la “Tume ya Amani” ya muda ya kuitawala Gaza. Tume hiyo itatekeleza majukumu yake kama vile kupokonya silaha kikamilifu katika Ukaknda wa Gaza, kutoa mafunzo kwa jeshi la polisi la Palestina, kufuatilia mipaka kati ya Misri na Israel, na kuwezesha misaada ya kibinadamu. China na Russia zinaamini kuwa chombo kama hicho kinaweza kuwa chini ya ushawishi wa moja kwa moja wa Marekani na Israel na kuwa wenzo kufanikisha maslahi yao katika eneo la Asia Magharibi.

2. Kufuta nafasi ya Wapalestina

Katika rasimu hiyo, Mamlaka ya Palestina haina jukumu lolote katika kusimamia kipindi cha mpito cha Gaza. Kwa mtazamo wa China na Russia, hii ina maana ya kupuuza haki ya Wapalestina ya kujiainishia mustakbali wao, na inaweza kuhoji uhalali wa kisiasa wa mpango huo.

3. Kulidhoofisha Baraza la Usalama

Wanadiplomasia wa Russia na China wamesisitiza kuwa kikosi cha kulinda amani kinapasa kufanya kazi chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa Baraza la Usalama, na si tume ya muda. Wamesema kuwa rasimu hiyo inadhoofisha nafasi ya Baraza la Usalama la UN na kwamba zaidi ya nusu ya yaliyomo hayako wazi na haikuzingatia masuala ya msingi muhimu.  

4. Ushindani wa kijiopolitiki na Marekani 

Upinzani wa China na Russia pia unaweza kuchambuliwa katika fremu ya ushindani wa kijiopolitiki wa nchi hizo mbili na na Marekani. Katika miaka ya hivi karibuni, nchi hizi mbili zimejaribu kupunguza ushawishi wa Washington katika maeneo nyeti duniani hasa eneo la Asia Magharibi. Upinzani dhidi ya mpango wa Marekani huko Gaza ni sehemu ya sera hii kuu.

Kwa kifupi ni kuwa: Upinzani wa China na Russia dhidi ya azimio lililopendekezwa na Marekani kuhusu Gaza unatokana na wasiwasi kuhusu ushawishi wa Washington na Israel, kufutwa nafasi ya Wapalestina, na kulidhoofisha Baraza la Usalama. Upinzani huu unaweza kuwa na athari muhimu kwa kile kinachotajwa kama mchakato wa amani na mustakabali wa Gaza. Hatua hii ina matokeo kama vile kushindwa kufikiwa muafaka kimataifa, kuendelea mgogoro wa binadamu na kuongezeka ushindani wa kijiografia-kisiasa kati ya Mashariki na Magharibi. 

Mwishoni tunaweza kusema kuwa upinzani huu unaonyesha kuwa mustakabali wa Gaza haufungamani tu na makubaliano ya ndani ya Palestina tu, bali pia na ushindani wa madola makubwa duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *