Wanafunzi 100 wa Shule ya Kikatoliki ya St Mary, Papiri ambao walitekwa wiki iliyopita, wameokolewa na vikosi vya usalama, huku 165 wakiwa hawajulikani walipo.

Mwenyekiti wa Chama cha Wakristo wa Nigeria (CAN) katika Jimbo la Niger, Askofu Bulus Dauwa Yohanna, pamoja na Kamishna wa Polisi wa jimbo hilo, Adamu Abdullahi Elleman, wameithibitishia BBC kuwa wamepokea taarifa rasmi kutoka Ofisi ya Mshauri wa Usalama wa Taifa kuwa kundi la kwanza la wanafunzi limepatikana wakiwa hai.

Kwa mujibu wa viongozi, watoto hao wanatarajiwa kuanza kuachiwa kwa makundi na kukabidhiwa kwa wazazi wao kuanzia leo Jumatatu Desemba 8,2025, hatua inayotoa matumaini mapya kwa familia zilizoendelea kusubiri kwa wasiwasi mkubwa.

Licha ya hatua hiyo, idadi kubwa ya wanafunzi bado haijapatikana. Taarifa zinaonyesha kuwa jumla ya wanafunzi 165 hawajulikani walipo, hali inayoongeza huzuni na taharuki miongoni mwa wazazi na jamii ya Papiri.

Matukio ya utekaji maeneo ya kaskazini mwa Nigeria yameendelea kuwa changamoto kubwa kwa mamlaka, huku wanaharakati na viongozi wa dini wakitoa wito wa kuimarishwa kwa usalama katika taasisi za elimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *