
Mwanadiplomasia mwandamizi wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu iliusababishia utawala wa kizayuni wa Israel uharibifu ‘mkubwa na ulioenea’ wakati wa uvamizi wake uliofanya mwezi Juni dhidi ya Iran kwa uungaji mkono wa Marekani.
Akizungumza jana Jumatatu, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran wa Sheria na Masuala ya Kimataifa, Kazem Gharibabadi alisema, wakati wa uvamizi huo, Iran ilitoa “kipigo kikali” kwa Israel, ambayo ilikuwa imeendelea kuwa na kiburi tangu vita vya miaka ya 1960, hasa Vita vya Siku Sita na migogoro iliyofuata baina yake na nchi za Kiarabu.
“Wakati wa vita, tuliutia hasara kubwa sana utawala wa Kizayuni, ni sehemu tu ambayo ilitangazwa hadharani. Israeli yenyewe ilizuia kufichuliwa kikamilifu kwa kiwango cha uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya makombora ya Iran”, ameeleza Gharibabadi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameendelea kueleza kwamba: “ripoti na picha tulizopokea kutoka satelaiti mbalimbali, pamoja na taarifa zilizopatikana kutoka vyanzo vingi katika maeneo yanayokaliwa na Israel, zote zilionyesha kuwa uharibifu uliopata utawala huo ulikuwa mkubwa sana.”
Amesema makombora ya Iran yalipenya kupitia mifumo mingi ya ulinzi iliyotumwa na nchi kadhaa kwa Israel kwa lengo la kuyaangusha makombora hayo yakiwa yako angani.
Gharibabadi amebainisha kwa kusema: “utawala wa Kizayuni unawakilisha nchi za Magharibi, hususan Marekani, kwa silaha zake zote.”
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefafanua kuwa, Israel inanufaika pia na kinga na ulinzi inaopatiwa na baadhi ya mataifa Ulaya na akongezea kwa kusema Vita vya Siku 12 havikuwa kati ya Iran na utawala wa Kizayuni tu bali mataifa yote hayo ya Ulaya yalihusika pia.
Utawala haramu wa Israel ulianzisha uchokozi wa wazi dhidi ya Iran mnamo Juni 13, na kuua watu wasiopungua 1,064 na kulenga miundombinu ya kiraia. Zaidi ya wiki moja baadaye, Marekani nayo ilikiuka sheria za kimataifa kwa kujiunga na vita hivyo na kulenga maeneo matatu ya nyuklia ya Iran.
Hata hivyo, mnamo Juni 24, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilifanikiwa kusimamisha uchokozi huo baada ya kutekeleza kwa mafanikio operesheni kali za kujibu mapigo na kulipiza kisasi dhidi ya utawala wa utawala na muitifaki wake mkuu Marekani.
Halikadhalika, Gharibabadi amesema, Israel haikufikia malengo yake ya kimkakati na ilishindwa vibaya, na kwamba hali ilifikia hatua ambayo Marekani yenyewe iliomba kusitisha mapigano…/