
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imeilaani vikali Israel kwa kutotimiza wajibu wake katika makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza, wakati harakati hiyo ya Palestina imetekeleza majukumu yake yote kwa mujibu wa awamu ya kwanza ya makubaliano hayo.
Abduljabbar Saeed, mwakilishi wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas amefafanua katika mahojiano na tovuti ya Quds News mijadala inayoendelea kuhusu awamu ya pili ya makubaliano ya kusitisha mapigano na suala la wapatanishi.
Amesema, pande zote zilizohusishwa katika makubaliano zimekubaliana kwamba utawala wa Israel haujatimiza majukumu mengi katika awamu ya kwanza ya usitishaji mapigano.
Amesisitiza kuwa, serikali ya Marekani ilishangazwa na utiifu wa Hamas, hasa kuhusiana na kurejesha na kukabidhi miili ya mateka wa upande wa Israel.
Mwakilishi huyo wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas amesisitiza kuwa Israel imeendelea kuwaua raia wa Palestina hasa watoto na wanawake huko Gaza katika awamu ya kwanza ya makubaliano.
“Familia za watu wa Gaza zimeachwa zikizama katika msimu wa baridi kufuatia kukosekana mahema yanayofaa kwa makazi, nyumba zinazohamishika na zana za kuondoa vifusi,” amesema Abduljabbar Saeed.
Ameeleza masikitiko yake kuwa, vifaa na bidhaa nyingi zinaoingizwa Gaza zinasambazwa na wafanyabiashara badala ya kupitia katika mkondo wa misaada ya kibinadamu.
Afisa huyo wa Hamas aidha amehoji, inawezekana vipi kusonga mbele na awamu ya pili ya makubaliano ya kusimamisha mapigano kabla ya Israel kutimiza ahadi na majukumu yake katika marhala ya kwanza ya utekelezaji wa makubaliano hayo?