
Wanafunzi 100 wa Nigeria waliotekwa nyara mwezi uliopita katika Shule ya Kikatoliki ya St. Mary’s huko Papiri katika eneo la Gongola hatimaye wamerejea nyumbani baada ya kuachiliwa mwishoni mwa juma.
Wanafunzo hao wameungana na familia zao zilizokuwa na hofu kubwa kuhusu hatima ya watoto wao baada ya kustahamili kwa wiki kadhaa.
Miongoni mwa walioachiwa huru kutoka mikononi mwa watekaji nyara ni mwanafunzi aliyejulikana kwa jina la Onyeka Chieme ambaye amesimulia hali ya kutisha ndani ya kambi ya watekaji nyara. Amesema, alihofia kuwa huenda asiweza kurejea nyumbani akiwa hai kwa kuzingatia sehemu waliyokuwa wakishikiliwa.
Masunura huyo anasimulia waliyokumbana nayo mikononi mwa watekaji nyara: “Tulipokuwa pale ( katika pango la watekaji nyara), waliwekuwepo watoto wengi chini ya uangalizi wa watekaji nyara ambapo mto ulikuwa chanzo pekee cha maji ya kunywa; yaani sehemu ileile ambayo wake na watoto wa watekaji nyara huenda kufua nguo zao. Baada ya kufua nguo zao, huchota maji yale yale na kulisha mifugo yao, na sisi pia tunapewa maji hayo hayo kwa ajili ya kunywa.”
Shambulio la Novemba 21 lilipelekea wanafunzi wasiopungua 303 na walimu 12 kutekwa nyara na watu wenye silaha katika mojawapo ya matukio makubwa ya utekaji nyara kuwahi kujiri tangu baada ya utekaji nyara katika shule ya Chibok, mwaka 2014.
Wakazi wa mji wa Papiri wanasema, magenge ya wahalifu waliojihami kwa silaha maarufu kwa kuwateka nyara wasafiri na watoto wa shule ili wapewe fidia, ndio yaliyohusika na shambulio hilo, ingawa hadi sasa hakuna kundi lililodai kuhusika rasmi na hujuma hiyo.
Licha ya taarifa hasi za utekaji nyara, lakini baadhi ya wazazi wanasema kuwa wamedhamiria kuwapa watoto wao elimu na kutoruhusu hofu na uoga kutawala miongoni mwao.
Nigeria imeathiriwa na matukio mtawalia ya kutekwa nyara wanafunzi mashuleni tangu mwaka 2014.