Waasi wa M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo jana Jumatano walitoa taarifa wakidai kuuteka mji wa kimkakati wa Uvira, ambao ni kitovu muhimu cha kibiashara karibu na mpaka wa nchi hiyo na Burundi.

Mji wa Uvira umekuwa ukitambuliwa kama makao makuu ya muda ya jimbo la Kivu Kusini tangu waasi wa M23 waidhibiti Bukabu mapema mwaka huu.

Vyanzo vya ndani vimeeleza kuwa waasi wa kundi la Machi 23 (M23) walielekea moja kwa moja katika mji wa Uvira yapata muda wa saa tano na nusu asubuhi kwa saa Kongo; na wakasonga mbele bila ya kukabiliwa na upinzani wowote wa jeshi la Kinshasa, wakielekea Kavimvira, katika mpaka na Burundi.

Vyanzo hivyo vimeeleza kuwa, sauti za ufyatuaji risasi zilisikika mapema jana na kwamba wanachama wa muungano wa waasi wa AFC/M23 wameonekana katika eneo la Kavimvira tangu Jumatatu kabla ya kuuteka mji wa kistratejia wa Uvira. 

Mapema Jumatano, Gavana wa Kivu Kusini, Jean-Jacques Purusi, alisema kuwa mji huo ungali unadhibitiwa na serikali. Hata hivyo Lawrence Kanyuka, msemaji wa waasi alidai katika ujumbe aliotuma katika mtandao wa X kwamba mji wa Uvira unadhibitiwa na M23. 

Kanyuka amewatolea wito raia wote waliokimbia mji huo kurejea nyumbani, akisema kuwa waasi M23 wapo mjini humo ili kuwalinda.

Jana vyanzo vya usalama viliiambia Redio ya Umoja wa Mataifa kwamba jeshi la Kongo lilirudi nyuma siku moja kabla ya kuelekea Swima, Makobola na Baraka katika eneo la Fizi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi,  Dr Edouard Bizimana jana alisema kuwa mpaka kati ya nchi hizo mbili bado uko wazi.

Waasi wa M23 hivi karibuni walisonga mbele katika maeneo kadhaa ya jimbo la Kivu Kusini licha ya makubaliano ya Desemba 4 kati ya Kongo na Rwanda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *