Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, sera za mataifa makubwa katika Asia Magharibi zimetengeneza “haki maalumu kwa ajili ya utawala wa Kizayuni,” hali ambayo imeiwezesha Israel kufanya uchokozi wa kijeshi katika eneo zima, ikiwa ni pamoja na dhidi ya Iran, bila kukabiliwa na mjibizo wa maana kimataifa kwa uchokozi wake huo.

Akihutubia Mkutano wa Kimataifa wa Amani na Uaminifu uliofanyika leo mjini Ashgabat nchini Turkmenistan, Rais Pezeshkian amesema, mazingira ya sasa ya kimataifa ya ubaguzi na kukosekana kwa usawa yameipa ruhusa Israel kuchukua hatua nje ya mipaka yaliyowekewa mataifa ya dunia.

“Katika mazingira yaliyopo ya ubaguzi na ukosefu wa usawa, sera ya mataifa makubwa katika Asia Magharibi kivitendo imeutengenezea upendeleo maalumu utawala wa Kizayuni,” ameeleza Rais wa Iran na kuongezea kwa kusema: “Upendeleo huu umekuwa chanzo cha vita vingi na kukosekana kwa haki katika eneo”.

Pezeshkian amebainisha kuwa, chanzo cha migogoro si cha kijeshi bali ni cha kimuundo, inayoundwa na mifumo ya kimataifa inayopendelea mataifa yenye nguvu kwa gharama ya mataifa dhaifu.

Amefafanua kwa kusema: “vita si matukio ya ghafla. Ni matokeo ya ubinafsi na hisia za kujiona bora. Hujikita katika miundo isiyo ya haki ya kiuchumi duniani, katika taasisi zinazopanua sauti za wenye nguvu na kunyamazisha za wanyonge, na katika mifumo ya kisheria inayoshurutisha haki kwa kuendana na matakwa ya mataifa makubwa”.

Mfumo kama huo, amesema Rais wa Iran, umeigeuza amani kuwa “fursa ya upendeleo maeneo fulani tu ya kijiografia” badala ya kuwa haki ya ulimwengu mzima.

Rais Pezeshkian ameendelea kueleza katika hotuba yake kwamba mchanganyiko wa mahesabu kijiopolitiki, maslahi ya usalama wa Magharibi na kufeli taasisi za kimataifa kiutendaji vimechangia kuipa hisia Israel ya kuwa na kinga ya kutoadhibiwa.

Hilo, -amesema-, limeupa kibali utawala wa kizayuni cha kutekeleza sera za kivamizi na kichokozi, akitolea mfano jinai zake za kila mara huko Ghaza, upanuzi wa vitongoji haramu katika Ukingo wa Magharibi na “mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya Syria, Lebanon, na pia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Qatar.”

“Mtendaji anapoachwa bila kuchunguzwa wala kufuatiliwa kimataifa, mizizi ya dhuluma hujikita na misingi ya amani endelevu hutoweka,” ameeleza Rais wa Iran.

Dk. Pezeshkian ameashiria uchokozi uliofanywa na Israel dhidi ya Iran mnamo mwezi Juni na akasema, shambulio hilo “liliwaua mamia ya wananchi wenzangu wasio na hatia” na likapata uungaji mkono wa kimataifa badala ya kulaaniwa.

Amekumbusha kuwa, ikiwa dunia inatafuta utulivu wa kudumu kusiwepo na nchi yoyote, hata mataifa makubwa, itakayopasa kuruhusiwa kujiweka juu ya sheria za kimataifa.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa wito wa kuitafakari upya maana ya amani, akisema usalama hauwezi kupatikana kupitia matumizi yanayoongezeka ya ulinzi au kwa miungano yenye nguvu kubwa…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *