
Shirika moja la kutetea haki za wanawake limesema, limerekodi matukio yapatayo 1,300 ya vitendo vya ukatili wa kingono na kijinsia vilivyofanywa katika vita vya ndani nchini Sudan huku Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) kikishutumiwa kuhusika na akthari ya vitendo hivyo.
Shirika la Mpango wa Kimkakati wa Wanawake katika Pembe ya Afrika (SIHA) jana Alkhamisi lilitoa ripoti ya matokeo ya uchunguzi wake na kueleza kwamba, limethibitisha jumla ya matukio 1,294 ya vitendo hivyo vilivyofanywa katika majimbo 14 tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipoanza nchini Sudan Aprili 2023.
Mtandao wa SIHA umehusisha asilimia 87 ya vitendo hivyo na wahalifu ambao wametambuliwa kuwa ni wapiganaji wa RSF, ukielezea ukiukwaji huo kama vitendo vinavyofanywa kwa sura ya kuenea, kujirudia mara kwa mara, kufanywa kwa makusudi, na mara nyingi kwa kuwalenga watu maalumu.
Ubakaji umetajwa kuwa umechangia zaidi ya robo tatu ya matukio yaliyosajiliwa, huku visa 225 vikihusisha watoto wadogo wenye umri hata wa miaka minne.
Ripoti hiyo imesema, ufichuzi huo unathibitisha jinsi ambavyo ukatili wa kingono umekuwa silaha ya kimfumo katika vita, ikiwa ni sehemu moja ya kutisha ya kile ambacho mashirika ya huduma za kibinadamu yamekiita hali mbaya zaidi ya kibinadamu kushuhudiwa duniani.
SIHA imefafanua kuhusu mfumo wa awamu tatu ambao utekelezaji wake umeambatana na kuvamiwa maeneo mbalimbali na kundi la RSF. Katika hatua ya kwanza, ni kufanywa uvamizi kwenye nyumba za watu pamoja na uporaji unaoambatana na ubakaji; ukifuatiwa na awamu ya pili ya mashambulizi katika maeneo ya umma sambamba na kuimarisha udhibiti; na hatimaye kuwaweka kizuizini wanawake kwa muda mrefu huku wakiteswa, kubakwa mtu mmoja na genge la watu na kufungishwa ndoa za kulazimishwa.
“Wanawake na wasichana kutoka makabila yasiyo ya Kiarabu huko Darfur, yakiwemo ya Masalit, Berti, Fur na Zaghawa, walilengwa moja kwa moja,” ripoti hiyo imesema…/