Bunda. Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya ametoa msaada wa vifaa vya shule kwa wanafunzi zaidi ya 300 wa shule za Msingi na Sekondari jimboni humo kwaajili ya kuwawezesha wanafunzi hao kuanza masomo katika muhula wa masomo wa 2026.

Msaada huo wenye thamani ya zaidi ya Sh41 unahusisha sare za shule,daftari, kalamu,viatu, soksi  pamoja na mabegi ya kubeba madaktari.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo kwa wanufaika hao mjini Bunda Januari 3,2025, Bulaya amesema suala la kutoa msaada kwa wanafunzi jimboni humo litakuwa ni endelevu huku akisema  lengo ni kuhakikisha wanafunzi hao wanapata fursa ya kupata elimu.

Amesema walengwa wa programu hiyo ni wale wanafunzi kutoka katika kaya masikini na wenye mazingira duni katika jimbo hilo huku akifafanua kuwa hakuna sababu ya mtoto wa kitanzania kukosa elimu kutokana na hali ya kiuchumi ya wazazi ama walezi wao.

Baadhi ya wazazi na watoto waliopokea msaada wa vifaa vya shule kutoka kwa mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya kwaajili ya kuanza masomo Januari 13,2026. Picha na Beldina Nyakeke

“Serikali inatoa elimu bila malipo ili watoto wote wa kitanzania wapate fursa ya kusoma sasa ni jukumu letu wadau kuunga mkono jitihada hizo kwa kutoa mahitaji muhimu kama daftari, kalamu,sare na vingine ili kuwawezesha watoto hasa kutoka mazingira duni kupata elimu kama ilivyo kwa wengine,” amesema.

Ametoa wito kwa wadau wilayani humo kushirikiana pamoja kwaajili ya kuwawezesha watoto wanaotoka katika mazingira magumu kupata elimu jambo ambalo kwa namna moja ama nyingine litasadia kuongeza idadi ya wasomi na wataalamu kutoka jimboni humo.

“Milioni 41 ni nyingi kwani ningeweza kutumia kwenye shughuli nyingine mfano ningewekeza kwenye kilimo lakini hatuna namna bora tujinyime starehe zingine ili  hawa watoto waende shule tutoe tulichonacho kwajili ya kutengeneza Bunda yenye  wataalamu wa baadaye,” ameongeza

Akikabidhi vifaa hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Bunda Aswege Kaminyoge ametoa wito kwa wadau na mashirika mbalimbali wilayani humo kujitokeza kwa wingi kusaidia wanafunzi wenye uhitaji ili waweze kupata elimu katika mazingira mazuri.

Amesema Serikali pekee haiwezi kufanikisha suala zima la masomo kwa wanafunzi hivyo ipo haja ya wadau hao kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha elimu nchini.

“Hatua zimechukuliwa ili watoto wa kitanzania waweze kupata elimu lakini bado zipo changamoto ambazo kwa namna moja ama nyingine zinahitaji ushirikiano wa wadau na jamii ili watoto wote waweze kupata elimu,” amesema

Amewataka wanafunzi waliopata msaada huo kuhakikisha kuwa wanasoma kwa bidii kwa maelezo kuwa elimu ni mwanga wa kufikia mafanikio ya aina yoyote.

Mkuu huyo wa wilaya pia amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanaripoti shuleni pale shule zitakapofunguliwa hata kama hawana mahitaji ya shule ikiwepo sare.

“Watoto wote kuanzia darasa la awali,la kwanza na kidato cha kwanza wanatakiwa kuanza masomo mara moja tena wafike kwa asilimia 100 hata kama hawana sare za shule,” amesema

Akizungumza kwa niaba ya wazazi, Lorencia Migato amemshukuru mbunge huyo kwa msaada huo na kusema changamoto ya ukata na ugumu wa maisha ni sababu ya  baadhi ya wazazi na walezi kushindwa kumudu gharama za mahitaji hasa vifaa vya shule pindi watoto wanapotakiwa kujiunga na masomo.

Amesema msaada huo ni ahueni kwao kwani mbali na kuwapunguzia mzigo lakini pia utawanusuru watoto wao kukatisha masomo kwa kukosa mahitaji.

Mmoja wa wasimamzi wa kituo la kulea watoto wanaoshi katika mazingira magumu kilichopo katika jimbo hilo, Mtawa Art Lleshaji amemshukuru Bulaya kwa moyo wake wa kujitolea, kujali ustawi wa jamii na kuendelea kuwa karibu na wananchi wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *