Waziri wa Katiba na Sheria, Juma Homera, ameupongeza Mkoa wa Morogoro kwa kile alichokiita “rekodi safi” ya kudumisha amani, akibainisha kuwa hakuna mkazi hata mmoja wa mkoa huo aliyekamatwa au kushiriki katika vurugu wakati wa maandamano ya Oktoba 29.

Akizungumza leo Jumatatu, Januari 5, 2026, katika viwanja vya stendi ya zamani mjini Morogoro, Waziri Homera amesema kuwa taarifa kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka zinathibitisha kuwa Morogoro ilibaki tulivu, huku wananchi wakiendelea na shughuli zao za maendeleo badala ya kushiriki fujo.

Waziri amempongeza Mkuu wa Mkoa, Adam Malima, kwa uongozi wake uliowezesha mkoa kubaki salama na kuimarisha mshikamano, jambo ambalo limefanya mkoa huo kuwa kimbilio la watu wanaotafuta utulivu.

Aidha, amebainisha kuwa utulivu huo ndio umekuwa chachu ya Serikali kuamua kuanza kutoa huduma za Kliniki ya Msaada wa Kisheria mkoani humo, kama sehemu ya mkakati wa kurejesha huduma kwa wananchi wanaozingatia sheria na taratibu za nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *