Kampuni Hodhi ya Mkulazi Sugar Company imekabidhi madawati 50 na printa mbili za kisasa kwa Shule ya Msingi Dumila Juu, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kurudisha kwa jamii inayozunguka kiwanda hicho.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa kitengo cha Mauzo na masoko wa Kampuni Hodhi ya Mkulazi, Goodluck Kway, amesema utoaji wa msaada huo ni utaratibu wa kawaida wa kampuni hiyo katika kuhakikisha jamii inayozunguka kiwanda inanufaika na uwepo wake.
“Tumeweza kukabidhi madawati 50 pamoja na printa mbili. Huu ni utaratibu wetu kama kampuni wa kurudisha kwa jamii, hasa katika maeneo yanayozunguka kiwanda chetu,” amesema Kway.
Ameongeza kuwa kampuni inaamini msaada huo utaongeza ushirikiano wa karibu kati ya jamii na kiwanda cha Mkulazi, huku akisisitiza kuwa kampuni hiyo imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kwa jamii na itaendelea kufanya hivyo ili kuhakikisha wananchi wananufaika na uwepo wa kiwanda hicho.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Dumila Juu Kayenze Senti Mjirio amesema kupokea kwa madawati hayo kumepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya uhaba wa madawati shuleni hapo.
“Tumepewa madawati 50. Awali tulikuwa na upungufu wa madawati 200, lakini sasa upungufu umepungua na kufikia madawati 150. Msaada huu umetusaidia sana,” amesema Mwalimu Mkuu.
Ameishukuru Kampuni ya Sukari Mkulazi kwa msaada huo akisema madawati na printa hizo zitasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
“Watoto watawakumbuka kila wanapokalia haya madawati. Kukaa kwenye dawati kunaongeza kujiamini kwa mwanafunzi, kunamwezesha kuandika kwa mwandiko mzuri na pia humkinga dhidi ya vumbi kwani hakai chini,” ameongeza.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Dumila Nyamunga Nyamunga amesema kijiji kitahakikisha kinayatunza madawati hayo ili yaweze kuwasaidia wanafunzi wengi zaidi kwa muda mrefu.
#KilichoBoraKabisa