Msemaji wa chama tawala cha Uganda, National Resistance Movement (NRM) amesema kuwa wapiga kura wa nchi hiyo wako tayari kumuunga mkono mgombea wa urais kutoka katika mazingira yoyote, mradi aonyeshe sifa zinazokubalika za uongozi.

Katika mahojiano ya kipekee na BBC, Emmanuel Lumala Dombo alisema kuwa historia ya mgombea, iwe ya kiraia au kijeshi, si kigezo pekee kinachoamua uamuzi wa wapiga kura.

Msemaji huyo wa NRM amesema kuwa kama wapiga kura wa Uganda wangekuwa wanazingatia wagombea wenye historia ya kijeshi pekee, basi wagombea wa aina hiyo wangekuwa wakipata uungwaji mkono mkubwa kila mara kuliko wengine.

Alitolea mfano mwanasiasa wa upinzani, Dkt. Kizza Besigye, ambaye aliwahi kuwania urais dhidi ya Rais Yoweri Museveni katika chaguzi zilizopita.

“Wakati Dkt. Kizza Besigye alipojitokeza kuwania urais dhidi ya Rais Museveni, baadhi ya watu walidhani angekuwa mgombea bora kutokana na historia yake ya kijeshi, lakini bado alishiriki uchaguzi na hakushinda,” alisema Dombo.

Kwa sasa, mmoja wa wagombea wanaoonekana kutoa changamoto kubwa katika uchaguzi ni mwanamuziki aliyegeuka mwanasiasa, Robert Kyagulanyi, anayefahamika zaidi kwa jina lake la kisanii, Bobi Wine.

Akizungumzia uvumi unaodai kuwa Rais Museveni anamuandaa mwanawe kama mrithi wake, Dombo alisema kuwa chama hicho kina taratibu zake za ndani kuhusu uongozi na urithishaji.

Aliongeza kuwa iwapo Jenerali Muhoozi Kainerugaba ataonyesha nia ya kuwania wadhifa wa kisiasa kupitia NRM, atalazimika kufuata taratibu na mchakato uliowekwa ndani ya chama hicho.

“Ikiwa Jenerali Muhoozi ataamua kutumia nafasi au uzoefu wake wa kijeshi, bado atalazimika kuthibitisha sifa nyingine zinazohitajika ili aonekane kama kiongozi anayestahili kuchaguliwa,” alisema.

Wananchi wa Uganda wanatarajiwa kupiga kura tarehe 15 Januari kuwachagua rais na wabunge wa bunge la taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *