
Wakazi wa kisiwa cha Greenland wameelezea wasiwasi wao kuhusu nia ya Marekani ya kujimilikisha kisiwa hicho kikubwa katika eneo la Aktiki, huku mijadala kuhusu mamlaka ya kujitawala ardhi hiyo ikipamba moto.
Wasiwasi huu ni ishara ya hofu iliyotanda miongoni mwa wenyeji wa Greenland kwamba nchi yao inaweza kuchukuliwa kama rasilimali ya kijeopolitiki. Wakazi wa Greenland wamesema kuwa Greenland si bidhaa ya kununuliwa na kwamba utamaduni na umoja wa ardhi ya kisiwa hicho vinapasa kuheshimiwa.
Wafanyabiashara ndani ya Greenland pia wameeleza wasiwasi wao kuhusu mashinikizo ya Marekani mkabala wa kisiwa hicho.
Serikali ya Trump imeeleza kile ilichokitaja kuwa wasiwasi wa kimkakati katika eneo la Aktiki na kuongezeka ushindani wa China na Russia; kwa msingi huo Washington inajiandaa kujadili suala la Greenland na Denmark, ingawa viongozi wa Ulaya wamepinga kikamilifu pendekezo lolote la Marekani la kuinyakua Greenland.
Msemaji wa White House, Karoline Leavitt alisema juzi Jumanne kwamba Trump ameeleza vyema kwamba kuimiliki Greeland ni kipaumbele cha usalama wa taifa wa Marekani, na kwamba “utumiaji wa jeshi la Marekani ni miongon mwa machaguo” yaliyoko mezani
Naye Avaaraq Olsen, meya wa Nuuk mji mkuu wa Greenland ameiambia televisheni ya Marekani ya CBC kwamba kisiwa hicho kilishuhudia maandamano makubwa katika msimu wa machipuo wakati wakazi wake walipojitokeza kwa wingi kupinga mipango ya Marekani ya kukidhibiti.
“Huo ndio msimamo wa watu Greenland”, amesema meya wa mji mkuu wa kisiwa hicho.