Ikulu ya Marekani, White House, imetangaza kuwa, Donald Trump ametoa amri ya kujitoa Marekani kwenye taasisi 66 za kimataifa ambazo Washington inadai kuwa hazitumikii tena maslahi ya Marekani.

Tangazo hilo limetolewa Jumatano, Januari 7, 2026. Donald Trump ametoa amri hiyo na kusema kuwa serikali yake haitolipa chochote kwenye taasisi hizo kuanzia sasa. Baadhi ya taasisi hizo ni zile za Umoja wa Mataifa. Amri hiyo ya Trump imevitaka vyombo vyote vya utendani vya Marekani vilivyokuwa vinadhamini fedha za taasisi 31 za Umoja wa Mataifa na 35 zisizo za Umoja wa Mataifa ziache mara moja kudhamini fedha hizo.

Taasisi nyingi zilizolengwa na uamuzi huu ni mashirika, tume na bodi za ushauri zinazohusishwa na Umoja wa Mataifa zinazofanya kazi katika sekta kama vile hali ya hewa, kazi na masuala mengine. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetangaza katika taarifa yake kwamba: “Utawala wa Trump umejiridhisha kuwa taasisi hizo ima zina mamlaka ya kujirudiarudia au hazidhibitiwi, au hazihitajiki au hazitumikii tena maslahi ya Marekani na nyingine zinahesabiwa kuwa ni tishio kwa uhuru na ustawi wa jumla wa Marekani.” 

Hiyo ni hatua ya hivi karibuni zaidi kuchukuliwa na Trump ya kuitoa Marekani kwenye taasisi za kimataifa. Huko nyuma serikali ya Marekani ilikuwa imeacha kusaidia taasisi nyingine za kimataifa kama vile Shirika la Afya Duniani, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwasaidia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO). 

Agizo la Trump la kuiondoa Marekani kwenye taasisi 66 za kimataifa linahesabiwa kuwa ni moja ya hatua kubwa zaidi za utekelezaji wa kile Trump anachodai ni Marekani Kwanza. Marekani inadai kuwa imefanya uchunguzi na kugundua kuwa, taasisi za kimataifa yakiwemo mashirika 35 yasiyo ya Umoja wa Mataifa na mashirika 31 ya Umoja wa Mataifa yanaendeshwa kinyume na maslahi ya kitaifa ya Marekani. 

Donald Trump, rais wa Marekani mwenye kiburi kupindukia

Zimetajwa sababu kadhaa zilizopelekea Trump kuchukua uamuzi huo:

Kwanza, utawala wa Trump unadai kuwa mashirika hayo hayana maana, hayafai na yametekwa na watendaji wanaotumikia maslahi ya nchi nyingine kwa kutumia rasilimali za kifedha na kidiplomasia za Marekani. Nyingi za taasisi hizi zinafanya kazi katika sekta kama vile mabadiliko ya hali ya hewa, uhamiaji, maendeleo, usawa wa kijinsia na sera za kijamii, ambazo utawala wa Trump unadai ni mambo ambayo yanapingana na uhuru na maadili ya Marekani.

Pili, Trump na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Marco Rubio wanadai kuwa mabilioni ya dola za ushuru wa wananchi wa Marekani zinatumiwa na mashirika hayo, wakati hakuna faida inayoonekana kwa Merekani.

Tatu, utawala wa Trump unadai kuwa umechukua hatua hiyo ili kurejesha uhuru wa kitaifa na kupunguza utegemezi wa Marekani kwa mifumo ya kimataifa. 

Lakini weledi wa mambo wanasema kuwa, athari mbaya za uamuzi huo ni kubwa na ni zenye matabaka mengi. Kwa upande wa ndani ya Marekani kwenyewe, Trump anaamini kwamba anaweza kuimarisha umaarufu wake wa kisiasa kwa sababu hatua yake hiyo inahudumia sera yake ya Marekani Kwanza. Pia inapunguza gharama za kifedha kwa serikali na kuzifanya zitumike kwa miradi ya ndani suala ambalo wachambuzi wa mambo wanatilia shaka uhakika na ukweli wake.

Amma katika ngazi ya kimataifa, kujiondoa Marekani kwenye idadi kubwa kiasi chote hicho cha taasisi za kimataifa kutadhoofisha ushirikiano wa kimataifa. Hii ni kwa sababu sehemu kubwa ya taasisi hizo zina jukumu muhimu la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuleta maendeleo endelevu, afya ya kimataifa na haki za binadamu. Kujitoa Marekani kunaweza kupunguza uwezo wa taasisi hizo kutekeleza majukumu yao na hivyo kuleta pengo ambalo mataifa mengine, hasa China, yanaweza kulijaza na kuzidi kuipotezea itibari Marekani. 

Suala jingine ni kwamba, hatua hiyo inawatia wasiwasi washirika wa Marekani ambao wanaliona jambo hilo kuwa ni ishara ya Washington kutojali mikataba na ahadi zake za kimataifa. Jambo hilo litazidi kupunguza imani ya mataifa ya dunia kwa Marekani na kuongeza ushawishi wa wapinzani wake wakuu kama China. Pia, miradi mingi ya maendeleo na ya kibinadamu ambayo ilikuwa inategemea misaada ya kifedha ya Marekani hivi sasa itakumbwa na hatari ya kufungwa au kupunguzwa kwa kiwango kikubwa shughuli zao. 

Agizo la Trump la kuitoa Marekani kwenye taasisi 66 za kimataifa linahesabiwa pia kuwa ni hatari ya kiusalama kwa Marekani yenyewe kwani weledi wa mambo wanasema kwamba, ijapokuwa agizo hilo linaweza kuwa na maslahi fulani ya kuongeza akiba ya fedha kwa serikali ya Marekani hivi sasa, lakini unapoangalia athari mbaya za muda mrefu utaona kuwa litapelekea kutengwa zaidi Marekani duniani; na mataifa ya dunia yataelekeza matumaini yao kwa mataifa mengine hasa yanayochipukia hivi sasa kimaendeleo na kuvuruga matunda ya miaka mingi Marekani ya kutafuta ushawishi duniani kwa gharama yoyote ile.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *