Dar es Salaam. Kila mwaka unaopofika ukingoni mamlaka ya kimataifa ya rangi – Pantone huchagua rangi ya mwaka unaofuata.

Kwa mwaka 2026 rangi ya ‘Cloud Dancer’ imechaguliwa kuwa rangi ya mwaka baada ya rangi ya ‘Mocha Mousse’ kutamba 2025.

Pantone imekuwa na utaratibu wa kuteua rangi ya mwaka kwa zaidi ya miaka 26 sasa ambayo husaidia kuongoza watu katika shughuli mbalimbali haswa za masuala ya mitindo.

Kwa mujibu wa tovuti mbalimbali za mitindo zinaeleza kuwa ili kufikia uamuzi wa kuteua rangi fulani kuwa ndiyo rangi ya mwaka wataalamu kutoka Pantone hufanya uchunguzi kwa muda fulani juu athari za rangi duniani na katika tasnia mbalimbali kama vile mitindo, burudani, filamu, uchoraji, upambaji, maeneo ya kumbi za sherehe, michezo, maeneo maarufu ya kusafiri pamoja na hali ya kiuchumi kwa wakati huo.

Pia inaelezwa kuwa huzingatiwa teknolojia mpya zinazogunduliwa nyenzo, yanayoathiri rangi, mifumo husika ya mitandao ya kijamii na hata matukio yajayo ya michezo yanayovutia watu duniani kote.

Inaelezwa kuwa uteuzi wa rangi huo unaofanyika kila mwaka imekuwa ina athari katika maamuzi ya mtu kununua vitu mbalimbali ikiwemo mavazi, vifaa vya majumbani, muundo wa picha, ufungaji na mambo mengineyo yanayohusisha rangi.

Cloud Dancer

Cloud Dancer kwa mujibu wa tovuti ya masuala ya urembo na mitindo ya ‘houseof beauty’, ni moja kati ya rangi zinazotokana na familia ya rangi nyeupe ikiwa na mng’ao hafifu.

Inaeleza kuwa katika saikolojia ya rangi inaziainisha rangi hizo zilizotokana na rangi nyeupe kuwa zinaashiria amani,utulivu na mwanzo mpya.

Kila mwaka rangi hizi hubeba ujumbe fulani kwa mwaka husika hivyo kwa mujibu wa tovuti ya Pantone rangi ya mwaka huu imebeba ujumbe unaosisitiza umuhimu wa amani, utulivu wa akili na nafsi.

Tovuti hiyo inaeleza kuwa rangi hiyo inahimiza umuhimu wa ‘kuanza ukurasa mpya’na kuachilia yale yaliyokuumiza katika miaka iliyopita.

Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya mitindo wanaeleza kuwa kuteuliwa kwa rangi fulani kuwa rangi ya mwaka kunasaidia watu kutotumia muda mrefu kutafuta rangi ambayo itatumika katika sherehe katika upande wa mavazi na mapambo.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Grace Mongi ambaye anaeleza kuwa watu wanapokuwa na sherehe haswa kwa upande wa wanawake wamekuwa wakiumiza kichwa ni rangi ipi wanaweza kuvaa lakini inapoteuliwa rangi fulani kuwa rangi ya mwaka inakuwa msaada kwao na kuwasaidia kuendana na wakati.

Grace anasema kuwa rangi iliyoteuliwa mwaka huu ni nzuri na inavutia haswa kwa watu wanaopenda rangi zilizopoa.

Pia anasema kuwa ni aina ya rangi ambayo inapatikana kwa urahisi.

Kwa upande wake Abduni Masud mkazi wa Kimara anasema masuala ya rangi ni ya wanawake kwa sababu huwa wana utaratibu wa kuwa na sare katika sherehe.”Wanaume kwa asilimia kubwa hatunaga desturi ya kuwa na sare katika shughuli hivyo masuala ya rangi ya mwaka yanawahusu zaidi wanawake.

Nae, Mwanaisha Juma anasema yeye huwa anazingatia kupendeza zaidi kuliko suala la rangi ya mwaka.

Akizungumza na Mwananchi fundi wa nguo za kiume na kike kutoka Kilumbi Fashion, Abdul Kilumbi anasema rangi iliyoteuliwa mwaka huu ni nzuri kwani inaweza kuvaliwa katika mazingira rasmi na hata shughuli nyingine za kijamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *