Dar es Salaam. Hatuzungumzi soka tunagusa sanaa na kipaji cha upekee cha Michel Kuka Mboladinga, maarufu kama Lumumba au Lumumba Vea. Mmoja wa mashabiki wa kipekee wa soka barani Afrika ambaye huwavutia wengi kwa tabia yake ya kushabikia akiwa amesimama bila kutikisika wakati timu ya taifa lake DR Congo ikicheza katika mechi za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 iliyofanyika nchini Morocco. Mfahamu zaidi

Mboladinga alizaliwa Septemba 26,1976 tangu utoto wake alionyesha shauku ya pekee kwenye soka pamoja na kupenda utamaduni na historia ya taifa lake.

Safari yake kama shabiki mwenye ushabiki wa kipekee ilianza mwaka 2013, alipochagua kujitolea kushabikia mechi za timu ya taifa kwa njia isiyo ya kawaida ya kuinua mkono wake wa kulia juu  huku akiwa amesimama bila kusogea muda wote wa mchezo ukiwa unaendelea yaani hujifanya kama sanamu.

Kipaji chake hicho cha kipekee kilivutia wengi na kumjengea jina kama shabiki ambaye haoneshi hisia zake wakati mchezo ukiendelea hata pale mpira ukiingia nyavuni. Tabia yake ya kushabikia bila kutikisika ilihusishwa na kumbukumbu ya kisiasa na kihistoria.

Ambapo Mboladinga huiga sanamu ya Patrice Lumumba, kiongozi wa uhuru wa Kongo na waziri mkuu wa kwanza wa taifa hilo baada ya uhuru mwaka 1960, ambaye anaheshimiwa kwa kujitoa kwake kwa taifa hasa kwa kupigania uhuru kwa taifa lake. Ikumbukwe Patrice Lumumba aliuawa mwaka 1961

Katika mechi kadhaa za AFCON 2025–26, Mboladinga ameendelea kujizolea umaarufu akiwa amevalia nguo zenye rangi za bendera ya DR Congo—bluu, njano na nyekundu. Huku akiwa amesimama kwa muda wote wa mchezo kama heshima na kumbukumbu ya sanamu maarufu ya Lumumba iliyopo Kinshasa.

Matendo yake yalikuwa tofauti kabisa na kelele na shangwe za mashabiki wengine waliokuwa uwanjani, wakicheza na kuimba. Aidha, Mboladinga alipewa heshima ya kipekee ya kusafirishwa pamoja na kundi la mashabiki wengine kadhaa waliolipiwa safari yao na serikali ya DR Congo kwenda Morocco, jambo linaloonyesha jinsi anavyo thaminiwa na kwenye taifa lake.

Kitu ambacho kimekuwa kikiwashangaza wengi kuhusu yeye ni ustahimilivu wake, kwani husimama bila kutikisika wala kubadilisha mkono hata wakati wa dakika za nyongeza, na mara nyingi alikuwa akionekana akitazama angani.

Licha ya kuwa DR Congo wametupwa nje ya michuano ya AFCON Mboladinga ameandika historia katika fainali za AFCON 2025 kwa kugeuka kivutio.

Ambapo ameweza kusimama jumla ya dakika 390 katika michezo minne. Mchezo wa hatua ya 16 bora DR Congo walicheza dakika 120 kabla ya kutolewa kwa bao la dakika za jioni lililofungwa na Boulbina wa Algeria. Na mwisho wa kuchapwa bao hilo Mboladinga alionekana kutokwa na machozi huku akiwa amesima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *