Jeshi la Israeli limesema siku ya Ijumaa kuwa linashambulia maeneo lengwa ya Hezbollah nchini Lebanon.
Jeshi la Lebanon limesema siku ya Alhamisi kuwa limechukua udhibiti wa operesheni kusini mwa nchi, lakini Israel ikajibu kuwa juhudi za kuwapokonya silaha wapiganaji wa Hezbollah hazitoshi.
Lebanon imekuwa chini ya shinikizo kubwa la kimataifa, hasa kutoka Marekani kuipokonya silaha Hezbollah, tangu makubaliano ya kusitisha mapigano mwezi Novemba 2024 yalipomaliza vita vya mwaka mmoja kati ya Israel na Hezbollah.
Jeshi lilisema lengo lake limefikiwa kwa “njia yenye ufanisi na inayoonekana” lakini bado kuna kazi ya kufanywa kuondoa silaha na handaki ambazo hazijalipuka.
Akijibu taarifa ya jeshi la Lebanon, ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ilisema juhudi za kuipokonya silaha Hezbollah kikamilifu zilikuwa “mwanzo wa kutia moyo, lakini hazitoshi, kama inavyothibitishwa na juhudi za Hezbollah za kujihami tena na kujenga upya miundombinu yake ya ugaidi kwa usaidizi wa Iran”.