Marekani. Mwigizaji wa Marekani, Jennifer Garner (53), amefunguka kile alichopitia baada ya talaka yake na aliyekuwa mumewe, Ben Affleck, (53), akieleza kuwa kuvunjika kwa familia yao ndilo lilokuwa jambo gumu zaidi.

Mastaa hao wanaofanya vizuri katika kiwanda cha filamu nchini humo (Hollywood), walitengana rasmi mwaka 2015 baada ya miaka 10 ya ndoa, huku talaka yao ikikamilika miaka mitatu baadaye.

Katika mahojiano na Jarida la Marie Claire UK wiki hii, Jennifer alizungumza kuhusu maisha yake ya sasa, na msimu wa pili wa tamthilia yake inayoruka Apple TV+, The Last Thing He Told Me.
“Kuvunjika kwa familia ndilo lilokuwa jambo gumu zaidi kwangu.

Kupoteza ushirikiano wa kweli na urafiki ndicho kilichokuwa kipindi kigumu kwa wakati huo,” alieleza Jennifer.
Hata hivyo, alieleza kuwa wakati wa kutengana kwao, alilazimika kutambua mipaka yake binafsi, pamoja na kukubaliana na uhalisia ya mambo ili maisha mengine yaweze kusonga mbele.

“Unapaswa kuwa mwerevu kuhusu kile unachoweza na usichoweza kukimudu, na mimi sikuweza kumudu mambo yaliyokuwa yakizungumzwa nje kuhusu jambo hii,” alisema na kuongeza.

“Lakini yale yaliyokuwa nje hayakuwa ndio magumu, bali kweli wenyewe ndio ulikuwa mgumu,” alieleza Jennifer, mama wa watoto watatu.

Baada ya kutengana na Affleck ambaye wana watoto watatu pamoja – Violet Anne, 20, Seraphina Rose, 17, na Samuel Garner, 13, Jennifer alijikita zaidi katika kudumisha uhusiano na watu wa karibu anaowaamini.

“Ninafanya juhudi kubwa sana kuwatembelea watu wangu kadri niwezavyo, kwa sababu hicho ndicho chenye maana. Hapo ndipo uimara wako ulipo; unakuwa na ukaribu na watu wanaokubeba na kukuvusha,” alisema.

Kuhusu maisha ya sasa, alisema vipaumbele vyake vikuu ni watoto, kazi za kijamii na uigizaji. Pia alikiri kuwa kulea watoto kwa pamoja na Affleck huku wote wakiwa watu maarufu limekuwa jambo lenye changamoto.

“Malezi sasa yamebadilika…. Unapaswa kuwaacha wakue na kufanya maamuzi yao. Huwezi kuyadhibiti, na hicho ndicho kitu kigumu zaidi,” alisema na kuongeza.

“Sio kigumu kwa kulinganisha na mambo magumu yanayoendelea duniani, lakini ni changamoto kwangu na kwa familia yangu kwa ujumla,” alisema Jennifer.

Hapo awali, chanzo kimoja kiliuambia mtandao wa People kuwa Jennifer na Affleck walisherehekea sikukuu ya Krismasi mwezi uliopita wakiwa pamoja na watoto wao.

Jennifer, staa wa filamu – The Rip (itakayoruka Netflix Januari 16), kwa sasa ana uhusiano na mfanyabiashara John Miller, huku akiendelea na kazi za kijamii kupitia mashirika ya Save the Children US na Once Upon a Farm.

Msimu wa pili wa tamthilia ya The Last Thing He Told Me unatarajiwa kuanza kuonyeshwa Apple TV+ hapo Februari 20. Pia Miongoni mwa miradi mingine ijayo kutoka kwake ni tamthilia ya Peacock The Five-Star Weekend.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *