
Rabat, Morocco. Manchester United wamepata habari njema baada ya Cameroon ya Bryan Mbeumo kutolewa kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) na Morocco.
Katika mchezo wa robo fainali, wenyeji Morocco walitinga nusu fainali baada ya kuwashinda mabingwa hao mara tano wa AFCON. Kwa vyovyote vile, Manchester United walijua kuwa mmoja wa wachezaji wao angeondoka mapema na kurejea England kuendelea na majukumu ya Ligi Kuu, na ni Mbeumo ambaye sasa anarejea kuiwahi Man City.
Habari hizi ni faraja kwa kocha wa muda Darren Fletcher, ingawa bado haijajulikana kama ataendelea kuwa kocha mkuu ifikapo Mbeumo atakapocheza mechi yake ijayo. Mabao ya Brahim Diaz na Ismael Saibari yaliizamisha Cameroon ya Mbeumo na kuwaondoa kwenye mashindano katika Uwanja wa Stade Prince Moulay Abdallah usiku wa Ijumaa.
Manchester United watakutana na wapinzani wao wa jadi Manchester City Jumamosi ijayo katika mechi ya mapema itakayochezwa Old Trafford. Mbeumo, mwenye umri wa miaka 26, ameanza vyema msimu wake wa kwanza Old Trafford baada ya kufunga mabao sita ya Ligi Kuu hadi sasa, na inaonekana ataingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza.
Kwa upande mwingine, Mazraoui ataendelea kubaki AFCON huku Morocco wakijaribu kushinda taji hilo mbele ya mashabiki wao wa nyumbani, wakiwa wamebakiza mechi mbili pekee kufanikisha ndoto hiyo.
Tangu wachezaji wa United waende AFCON, klabu hiyo imemfuta kazi kocha Ruben Amorim na sasa iko katika mchakato wa kuchagua kocha wa muda. Sir Jim Ratcliffe na uongozi wake wanawatazama Michael Carrick na Ole Gunnar Solskjaer, huku Darren Fletcher pia akitajwa kuwa na nafasi ndogo.
Kwa mujibu wa Daily Mail Sport, Solskjaer atafanya mazungumzo ya ana kwa ana na Manchester United siku ya Jumamosi. Carrick, mwenye umri wa miaka 44, alikutana na Afisa Mtendaji Mkuu Omar Berrada pamoja na Mkurugenzi wa Michezo Jason Wilcox Alhamisi, huku Solskjaer akipangwa kufanyiwa mahojiano yake Carrington Jumamosi.
Ingawa kuna uvumi kuwa Solskjaer ndiye kipenzi cha wengi, klabu imekuwa ikimpa uzito mkubwa Carrick, ambaye aliwahi kuwa kocha wa timu ya kwanza chini ya Solskjaer kati ya 2018 na 2021, na pia aliwahi kuwa kocha wa muda baada ya Solskjaer kufutwa kazi. Hata hivyo, wazo la wao kufanya kazi pamoja tena limeondolewa.