Huenda Klabu ya Wydad Casablanca walivutiwa na kiwango alichokionyesha Seleman Mwalimu ‘Gomez’ katika michezo miwili ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 yanayoendelea huko Morocco, baada ya kuthibitisha uwezo alionao wakati alipoitumikia timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars katika mechi mbili za mashindano hayo makubwa Afrika.

Mwalimu aliingia kwa mara ya kwanza dimbani katika mechi dhidi ya Tunisia iliyopigwa Desemba 30, 2025. Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdallah jijini Rabat ndiyo siku ambayo Stars iliandika historia ya kutinga hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza tangu ianze kushiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza mwaka 1980 nchini Nigeria.

Katika mchezo huo, Mwalimu aliingia akitokea benchi kuchukua nafasi ya nahodha, Mbwana Samatta dakika ya 44 huku ikishuhudiwa Stars ikipata matokeo ya sare ya bao 1-1 ambayo yaliivusha hadi hatua ya robo fainali ambapo ilishindwa kufurukuta mbele ya wenyeji wa mashindano Morocco na kutupwa nje baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0.

Katika mchezo huo wa 16 Bora, Mwalimu alionekana kuwa mwiba mchungu kwa mabeki wa Morocco ambao walipata wakati mgumu sana kumdhibiti nyota huyo wa Wydad Casablanca anayekipiga Simba kwa mkopo. Kipindi cha pili dakika ya 55 Mwalimu alimtengenezea nafasi ya kufunga kiungo, Feisal Salum ‘Fei toto’ ambaye alishindwa kuuweka mpira kambani.

Hata hivyo, licha ya kutopachika bao lolote kwenye mashindano hayo, mshambuliaji huyo bado alionyesha kiwango bora ambacho pengine kinaweza kuwashawishi mabosi wake, Wydad Casablanca kufikiria kumrudisha kwenye timu baada ya mkataba wake wa mkopo kumalizika huko Msimbazi katika majira ya kiangazi mwaka huu.

Januari 31 mwaka jana nyota huyo alitambulishwa kwa mabingwa hao wa zamani wa Ligi ya Mabingwa Afrika akitokea Fountain Gate alikokuwa anacheza kwa mkopo kutoka Singida Black Stars kwa mkataba wa miaka mitatu. Mechi yake ya kwanza ilikuwa Februari 22 akicheza kwa dakika 31 dhidi ya COD Meknes, Wydad ikitoa suluhu.

Rekodi yakipekee

Mwalimu aliandika rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kucheza katika michuano ya Kombe la Dunia la Klabu lililofanyika Marekani Juni mwaka jana. Katika mechi hiyo ya kundi G, iliyopigwa Juni 22, 2025 kwenye Uwanja wa Lincoln Financial jijini Philadelphia, Wydad ilichapwa mabao 4-1 na Juventus ya Italia ambacho kilikuwa ni kipigo cha pili mfululizo, baada ya awali kuchapwa 2-0 na Manchester City ya England.

Alipozungumza baada ya mchezo huo kumalizika, Gomez alisema kitendo cha kupata nafasi ya kucheza michuano hiyo mikubwa ni heshima kubwa kwake, kwani itabaki katika historia na kumbukumbu nzuri ya maisha yake ya soka.

“Imeniuma kwa sababu tumepoteza mechi mbili mfululizo ila sijaangalia sana hilo, isipokuwa nilichohitaji ni kupata fursa ya kucheza katika michuano hii mikubwa, kwangu imeniongezea morali ya kuamini kila kitu kinawezekana,” alisema Gomez.

Katika dakika 45 alizocheza nyota huyo dhidi ya Juventus, kwa mujibu wa mtandao wa FotMob, aligusa mpira mara 15, akapiga pasi sita (6/6) ambazo zilifika zote kwa usahihi wa asilimia 100, alipiga shuti moja lililolenga lango la wapinzani  (1/1) kwa usahihi wa asilimia 100 pia na kutengeneza nafasi ya hatari moja.

Takwimu za Gomez zilionyesha amepata alama 6.8, akiwa mchezaji wa tatu wa Wydad aliyepewa alama nyingi katika mchezo huo baada ya mfungaji wa bao pekee Thembinkosi Lorch (7.7) na Nordin Amrabat (7.4) ambao walicheza kwa dakika zote 90.

Gomez wakati anajiunga na Wydad, alikuwa amefanya vizuri katika Ligi Kuu Bara alipokuwa akiitumikia Fountain Gate kwa mkopo akifunga mabao sita.

Alivyoondoka Morocco

Mwalimu alitambulishwa kujiunga rasmi na Simba Agosti 28, kwa mkopo wa msimu mmoja akitokea Wydad Casablanca.

Akizungumzia kuhusu usajili wake ndani ya klabu ya Simba, Mwalimu alisema amekuja kwa kazi maalumu huku malengo yake yakiwa sio kurudi tena nyuma bali ni kwenda mbele zaidi.

“Nimekuja kama mwanajeshi aliyeko vitani nina kazi maalumu ambayo nimekuja kuifanya kwa sababu malengo yangu siyo kurudi tena nyuma nataka niende mbele na njia ambayo nimechagua ni kuja hapa, kisha niondoke tena,” alisema.

Sababu kutua Simba

Mwalimu alielezea jinsi usajili wake kuja Simba ulivyokuwa licha ya uongozi wa Wydad kuonesha ugumu wa kumwachia aondoke.

“Wakati nimeenda Wydad nilitoka timu ya daraja la chini ambayo ni Fountain Gate lakini nilivyofika kule niliaminika nikawa nacheza na nilifanya vizuri kila mechi niliyopewa nafasi.

“Kipindi Simba wanatuma ofa ya kunihitaji kocha alikuwa hataki na viongozi walikuwa hawataki. Simba walituma ofa mara mbili na zote zilikataliwa lakini kocha Fadlu aliongea na uongozi wangu na akaonyesha nia ya kunitaka.

“Niliongea na kocha wangu wa Wydad kuhusu kutaka kuondoka, lakini alinikatalia akaniambia bado ananihitaji, nilimwambia nahitaji nafasi ya kutosha kucheza zaidi na ninayopata hapa, alinikubalia kwa kuwa bado nina miaka minne ya kucheza Wydad, kwa hiyo mimi ndiyo nilifanya mambo yakawa rahisi,” alisema Mwalimu.

Waliosema kuwa amefeli

Mwalimu hakukaa kimya kuhusu watu wanaomsema kuwa amefeli kucheza Wydad;

“Huo ni mtazamo wao lakini mimi najua ni kitu gani ambacho kimenifanya nimekuja Tanzania na malengo ambayo nimejiwekea mimi mwenyewe katika msimu huu wa 2025/2026. Nimekuja kwa mkopo wa mwaka mmoja lakini huwezi jua kama Wydad pengine wakanihitaji tena kwenye dirisha dogo hata kabla ya mwaka kumalizika.

“Kwa hiyo mimi najua kitu ambacho kimenileta Tanzania na najua kazi iliyonileta. Binafsi sina presha yoyote kutokana na maneno ya watu kwenye mitandao, huwa nachukulia kama changamoto ambayo inanipa motisha kwenda kuwaonyesha ubora wangu uwanjani.

“Mimi nitawaonyesha na watajua kweli kijana amekuja kwa malengo gani, kwa hiyo nitapambana kadiri ya uwezo wangu kuhakikisha naisaidia timu kwa asilimia mia moja.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *