Dar es Salaam. Ndani ya Bongofleva kuna wasanii wachache wenye uwezo wa kuimba na kucheza kwa umahiri, miongoni mwa Nedy Music ambaye kwa miaka takribani 10 sasa ameendelea kuifanya kazi hiyo kwa bidii.

Siku zote anasifika kwa sauti laini na melodi tamu zimeunganishwa na simulizi za kila siku kuhusu mapenzi na utamaduni wa kule anapotokea. Na huyu ndiye Nedy Music.

1. Aliingia katika tasnia akiwa kama dansa ambapo pamoja na kundi lake waliibuka washindi wa shindano la Dance La Fiesta 2010, na baadaye alishiriki mashindano ya Dance Mia Mia 2012 ila hawakufanya vizuri.

2. Baada ya kuhitimu sekondari mwaka 2013, Nedy alipenda kujifunza zaidi muziki ndipo akajiunga na Tanzania House of Talent (THT) kwa kipindi kama ilivyokuwa kwa Marioo ambaye naye alipita hapo.

Mbali na Nedy na Marioo, kuna mastaa wa Bongofleva waliowahi kunoa vipaji vya ndani ya THT ila hakuwatoka kimuziki chini ya chapa hiyo, baadhi yao ni Ben Pol na Maua Sama.  

FAC 01

3. Nedy ndiye msanii wa kwanza kusainiwa na lebo ya Ommy Dimpoz, Poz kwa Poz (PKP) Entertainment, kisha akatambulishwa kupitia wake, Usiende Mbali (2016) ambao alimshirikisha Bosi wake huyo.

4. Wimbo huo ulitayarishwa na Nahreel huku video ikiongozwa na Justin Campos kutokea Afrika Kusini. Kwa kiasi chake ulifanya vizuri ukikamata chati za vituo vikubwa kama Trace, MTV Base na Sound City.

5. Baada ya Nedy kuondoka PKP, hadi sasa lebo hiyo hajawahi kumsaini mwanamuziki mwingine!. Hata hivyo, PKP si lebo ya kwanza ya staa wa Bongofleva kuacha kusaini wasanii baada ya kumtambulisha wa kwanza.
Kumbuka Next Level Music (NLM) yake Rayvanny, hii kufuatia aliyekuwa msanii wake, Mac Voice ‘kujiweka kando’ hadi sasa NLM haijatambulisha msanii mwingine tena.  

FAC 03

6. Moja ya sababu zinazotajwa kumuondoa Nedy ndani ya PKP, ni kufuatia Ommy Dimpoz naye kusainiwa na RockStar Africa (2017) na baadaye Sony Music Entertainment Africa hapo 2017.

7. Baada ya kufanya vizuri na wimbo wake, One and Only (2018) akimshirikisha Ruby, Nedy alishinda tuzo ya All Africa Music Award (AFRIMA) 2018 akiwa ni msanii wa kwanza kutokea Zanzibar kufanya hivyo.

Cha kufurahisha ni kwamba huu ndio uliokuwa wimbo wa kwanza kuachia tangu kuachana na PKP, na kati ya wasanii aliokuwa anawania nao tuzo hiyo ni pamoja na aliyekuwa Bosi wake, Ommy Dimpoz (Yanje).

8. Katika muziki Nedy amejipachika a.k.a ya Mpemba Mmoja ili kujivunia na kuwakilisha kule anapotokea kama ilivyo kwa Mike Tee (Mnyalu), Fid Q (Ngosha The Swagga Don) au Mimi Mars (Chuga Queen).

FAC 04

9. Video za nyimbo za Nedy ambazo zimefanikiwa kutazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 1, ni zile alizowashirikisha wasanii wenzake, huku zile alizoimba peke yake (solo) zikishindwa kufikia rekodi hiyo.

Nyimbo hizo ni Nishalewa (2017) ft. Mr. Blue, One and Only (2018) ft. Ruby, Usiende Mbali (2016) ft. Ommy Dimpoz, na Rudi (2016) ft. Christian Bella, mwanamuziki mwenye asili ya DR Congo.

10. Tangu ametoa kimuziki, Nedy Music hajawahi kutoa albamu bali amefanikiwa kuachia Extended Playlist (EP), The Voice Of The Island (2025) yenye nyimbo sita za Afro-Pop zilizosheheni ladha ya visiwani.

EP hii inayoakisi maisha na utamaduni visiwani, imetayarishwa na Dracko Beats na kurekodiwa studio ya The Sound Lab. Kwa sehemu kubwa inaonyesha ukuaji wake kisanaa akiibeba kikamilifu ladha yake ya Kizanzibari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *