Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty amesema, nchi yake itachukua hatua zote zinazohitajika ili kuhifadhi umoja wa ardhi ya Sudan, wakati nchi hiyo jirani inakaribia kuingia mwaka wake wa nne wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyohusisha vikosi vya jeshi SAF na vile vya usaidizi wa haraka, RSF.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Sudan, Ramtane Lamamra, Abdelatty amesema, Misri “haitakaa kimya wala kusita kuchukua hatua zinazohitajika ili kuilinda Sudan, mamlaka yake na umoja wa ardhi yake”.

Misri inapakana na Sudan upande wa kusini, na ni mmoja wa washirika wa karibu wa jeshi la Sudan, ambalo limekuwa likipigana na RSF tangu Aprili 2023.

Abdelatty amesisitiza kwamba, Misri “haitakubali wala kuruhusu kwa hali yoyote kuanguka kwa Sudan, kuanguka kwa taasisi za kitaifa za Sudan au kuharibiwa umoja wa Sudan.”

“Huu ni mstari mwekundu,” amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, akiongeza kuwa “kuvunja usalama wa taifa la Sudan ni kuvunja usalama wa taifa la Misri”.

Matamshi hayo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri yanafanana na yale yaliyotolewa na rais wa nchi hiyo Abdel Fattah al-Sisi wakati wa mkutano wa mwezi uliopita na Mkuu wa Jeshi la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.

Wakati wa mkutano huo, al-Sisi alisisitiza pia kuwa tishio lolote kwa taasisi za serikali ya Sudan ni kama “mstari mwekundu kwa Misri.”

Misri na Sudan zina historia ndefu ya ushirikiano wa kijeshi. Mnamo Machi 2021, zilisaini makubaliano yanayohusu mafunzo, usalama wa mipaka na juhudi za pamoja dhidi ya vitisho vya pamoja, ikiwa ni utekelezaji wa mkataba wa ulinzi wa 1976 uliolenga kukabiliana na hatari za nje…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *