Tarehe 12 Januari (Dei 22) ni ukumbusho wa siku ambayo wanajeshi wa Marekani walitekwa na majeshi ya Iran katika Ghuba ya Uajemi.
Tarehe 12 Januari, 2016 (Dei 22) ni ukumbusho wa siku ambayo majeshi ya Marekani yalitekwa na majeshi ya Iran katika Ghuba ya Uajemi, wakati boti mbili za kivita zilizobeba askari 10 wa Marekani zilipoingia kwenye maji ya Iran. Boti hizo za Marekani zilikuwa zimeingia kilomita 2 ndani ya maji ya Iran zilipokamatwa na askari wa majini wa jeshi la Iran IRGC.
Hivyo, wakati Rais Barack Obama wa Marekani, alipokuwa akipiga nara na kudai katika Bunge la Congress kwamba nchi hiyo ndiyo yenye “nguvu zaidi” duniani, umbali wa kilomita elfu 11 katika Ghuba ya Uajemi, wanajeshi 10 wa Marekani walikuwa wanapigishwa magoti na vikosi vya Brigedi ya 214 ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran IRGC. Wanajeshi hao, wakiwemo wanaume tisa na mwanamke mmoja, walihamishiwa kwenye moja ya vituo vya IRGC katika Kisiwa cha Uajemi. Asubuhi ya Januari 13 (23 Dei), Jenerali Ali Fadavi, kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu alitangaza kwamba: ‘Baada ya kukamatwa boti hizi, tuliona Jeshi la Wanamaji la Marekani na manowari moja ya nchi hii zikidhihirisha tabia isiyo ya kitaalamu kwa muda wa dakika 40 ambapo walifanya harakati hatari za anga na majini katika eneo, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa Marekani haijali usalama na amani ya eneo.’
Hatimaye Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilitangaza kuachiliwa huru wanajeshi hao wa Marekani katika maji ya kimataifa baada ya kuthibitisha kwamba kuingia kwao katika maji ya Iran kulifanyika kimakosa na bila kukusudia. Tukio hili lilikuwa fedheha kubwa kwa Wamarekani ambao walidhani kwamba wangeweza kuingia katika ardhi ya Iran bila ruhusa, wakati majeshi ya Iran yalikuwa macho yakilinda vilivyo maji, ardhi na anga ya Iran na kufuatilia mienendo ya majeshi ya kigeni.
Meja Jenerali Ramazan Zirahi, kamanda wa wakati huo wa eneo la pili la Jeshi la Wanamaji la IRGC, aliashiria mafanikio ya tukio hilo muhimu kwa kusema: ‘Mafanikio makubwa zaidi ya kukamatwa kwa Wanamaji wa Marekani ni kuvunja kiburi na majigambo ya Marekani katika eneo na dunia nzima.’ Alifafanua zaidi ukubwa wa tukio hilo la kudumu milele na kulifungamanisha na kauli ya Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Iran, ambaye alisema, “Tukio hili ni kazi ya Mwenyezi Mungu.”

Tunaweza kusema kuwa hivi sasa, baada ya kupita miaka 10 tangu tukio hilo la kihistoria ambalo lilifedhehesha Marekani na jeshi lake katika kieneo na kimataifa, rais mwenye chuki na mpenda vita wa Marekani Donald Trump, sasa anataka kulipiza kisasi dhidi ya Iran ya Kiislamu. Katika muhula wa pili wa uongozi wake, Trump amezidisha siasa na hatua za uhasama dhidi ya Iran, na hasa katika wiki chache zilizopita, ambapo Marekani na Israel, zimeingilia na kuhochea machafuko ya magenge ya vurugu na mauaji dhidi ya mfumo wa Kiislamu.
Trump na maafisa wa serikali yake wamekuwa wakizungumza mara kwa mara hadharani kuhusu kubadili tabia au hata kubadili mfumo wa kisiasa nchini Iran, jambo ambalo linachukuliwa kuwa ishara tosha ya kuchochea ukosefu wa utulivu na machafuko nchini. Kauli za Trump kuhusu “chaguo kali sana” dhidi ya Iran na uwezekano wa kuchukuliwa hatua za kijeshi kwa kisingizio cha machafuko nchini Iran na kuwaunga mkono wafanya ghasia zimekuwa zikikaririwa mara kwa mara kuhusiana na suala hilo. Licha ya vitisho hivyo vyote, lakini Trump amelazimika kulegeza msimamo na kuachana na vitisho hivyo kwa sasa. Msimamo thabiti wa Iran dhidi ya vitisho vya Marekani na sisitizo la kukabiliana navyo vilivyo ni moja ya sababu muhimu ambazo zimemlazimisha Trump kurudi nyuma. Inasemekana washauri wake wamemuonya juu ya madhara ya hatua za kijeshi dhidi ya Iran na kumzuia kuchukua hatua ya kipumbavu kama hiyo.
Washauri hao wametilia shaka kudhoofishwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia hatua ya kijeshi ya Marekani. Kwa upande mwingine, wamemuonya juu ya Marekani kutokuwa na uwezo wa kukabiliana na jibu kali la kijeshi la Iran. Inaonekana kuwa kwa sasa rais mwenye chuki kali wa Marekani dhidi ya Iran ambaye daima anaota ndoto ya kuishambulia kijeshi Iran amelazimika kujiepusha na vitisho vyake vya kijeshi dhidi ya taifa la Iran, kutokana na maonyo makali ya Iran kwa upande mmoja na upinzani wa washauri wake wa kijeshi na kiusalama na vile vile nchi za eneo kwa upande wa pili.