Vyombo vya habari vya utawala ghasibu wa Israel sanjari na kuchapisha ripoti mbalimbali, vimekiri juu ya taathira ya operesheni za vikosi vya muqawama vya Yemen kwa uchumi wa utawala huo.
Kanali ya 14 ya Televisheni ya Israel imefichua katika ripoti yake kwamba: Kupuuzwa bandari ya Umm al-Rashrash (Eilat) kumekuwa kukiendelea kwa zaidi ya miaka miwili sasa kutokana na kuendelea operesheni za vikosi vya Yemen wakati wa vita vya Gaza na ukosefu wa uwajibikaji wa baraza la mawaziri la Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.
Ripoti hiyo inasema kwamba, onyo limetolewa kuhusu kufukuzwa kazi wafanyakazi 130 katika bandari ya Eilat, na kwamba viwanda vyote vya Israel vinapata hasara kubwa kutokana na baraza la mawaziri kutoweza kutekeleza mpango wa usaidizi wa bandari hiyo kutokana na hasara kubwa inayopata.
Hapo awali, jarida la kiuchumi na biashara la Kizayuni la “Calcalist” pia lilifichua kwamba, faida ya Shirika la Usafiri wa Majini la Israel (ZIM), imepungua kutokana na operesheni za uungaji mkono za jeshi la Yemen kwa Gaza na mzingiro wa jeshi la majini la utawala huo.
Jarida la Calcalist pia liliripoti kwamba, nakisi ya biashara ya Israel imefikia rekodi ambayo haijawahi kushuhudiwa. Gazeti hilo liliripoti kwamba, kulingana na takwimu za Kituo cha Takwimu cha Israel, nakisi ya biashara ya bidhaa mwaka 2025 ilifikia dola bilioni 38, ikiwa ni ongezeko la asilimia 20 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake (2024).
Kile ambacho vyombo vya habari vya Israel vimechapisha kinaonyesha kwamba, operesheni za majini na makombora za Yemen hazijawa na mwelekeo wa kijeshi tu, bali pia zimekuwa na athari kubwa na hasi kwa Uchumi wa utawala wa Israel. Athari za operesheni za muqawama wa Yemen zinaweza kuonekana katika nyuga tatu: Kuvurugika kwa njia na bandari za biashara, uharibifu kwa makampuni ya usafirishaji na mnyororo wa usambazaji wa bidhaa, na kuongezeka kwa mgogoro wa nakisi ya biashara na kupungua kwa mauzo ya nje ya utawala wa Israel.

Bandari ya Eilat, kusini mwa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu kivitendo haitumiki kwa zaidi ya miaka miwili sasa. Sababu kuu ya hili ni kuendelea kwa operesheni za kijeshi za vikosi vya muqawama wa Yemen na kutoweza utawala wa Kizayuni kukabiliana na mwenendo huu. Viwanda mbalimbali vya utawala wa Kizayuni pia vimepata hasara kubwa kutokana na kusitishwa kwa shughuli za Bandari ya Eilat.
Katika kujibu unyama wa Israe, vikosi vya muqawama vya Yemen viliingia katika medani ya vita kuwaunga mkono wananchi wa Gaza na kuendelea na operesheni zao kubwa katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Bahari Nyekundu na kutoa pigo kubwa kwa utawala wa Kizayuni. Wayemeni wamesisitiza kwamba operesheni zao dhidi ya utawala wa Kizayuni zitaendelea hadi utawala huo ghasibu utakapokoma kukalia kwa mabavu Ukanda wa Gaza.
Operesheni ya Wayemen katika Bahari Nyekundu imeanzisha vita kamili vya kiuchumi dhidi ya utawala wa Kizayuni. Sambamba na hali hii ya mgogoro kwa utawala wa Kizayuni, pia imeleta nakisi ya biashara kwenye rekodi ya kihistoria na kupunguza mauzo ya nje hadi kiwango cha chini kabisa katika miongo kadhaa ya hivi karibuni. Vikosi vya muqawama vya Yemen vimetoa pigo kubwa zaidi la kiuchumi kwa utawala wa Kizayuni kwa gharama ndogo zaidi; pigo ambalo hata vyombo vya habari vya utawala vimelazimika kukiri waziwazi.
Kile ambacho muqawama wa Yemen umekifanya kivitendo kimebadilisha mlingano wa nguvu katika Bahari Nyekundu na mashariki mwa Mediterania. Utawala wa Kizayuni umefikia hatua ambayo, licha ya himaya na uungaji mkono kamili wa Wamarekani na Magharibi na uwepo wa meli za kijeshi za Marekani katika eneo hilo, usalama wake wa baharini umeharibiwa vibaya, na vikosi vya muqawama vya Yemen vimekuwa mchezaji mkuu katika matukio katika eneo hilo.
Operesheni za majini za vikosi vya muqawama vya Yemen zimeonyesha kuwa, mhusika wa kikanda anaweza kuathiri mtiririko wa biashara ya kimataifa, usalama wa baharini, na uchumi wa Israel. Mwelekeo huu umeinua nafasi ya Yemen katika milingano ya usalama wa Bahari Nyekundu na hata siasa za Asia Magharibi.