
Iran siku ya Ijumaa ilipinga kikao maalum cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC), ikikitaja kuwa hakina uhalali. Mjumbe wa Iran mjini Geneva alisisitiza kwamba Iran halijawahi na halitakubali kutawaliwa au kushinikizwa na nguvu za kigeni.
Balozi wa Iran na mwakilishi wa kudumu katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Ali Bahreini, ametoa kauli hiyo Ijumaa wakati akihutubia Kikao Maalum cha 39 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuhusu Iran.
Amesema, “Taifa la Iran, lenye ustaarabu wa zaidi ya miaka 2,500, halijawahi kukubali utawala wa mabavu au ukoloni.” Ameongeza kwamba, “Historia imethibitisha mara kwa mara kuwa Iran haikubali shinikizo la kigeni, wala haitovumilia mashinikizo ya kificho yanayojificha nyuma ya mwavuli wa ‘wasiwasi.’”
Aidha, amebainisha kuwa wananchi wa Iran wamepitia vita, vikwazo, ugaidi na misukosuko isiyokoma, lakini bado wamesimama pamoja kwa umoja na uthabiti.
Amesisitiza kwamba, “Ni jambo la kushangaza kwa kiwango cha kina kwamba mataifa ambayo historia yao imechafuliwa na uhalifu wa kivita, mauaji ya kimbari, na mifumo ya ukatili, hata dhidi ya raia wao wenyewe, leo hii yanajipa mamlaka ya kuifundisha Iran kuhusu utawala wa kijamii na haki za binadamu.”
Mjumbe huyo aliongeza kuwa wale waliodhamini kikao hicho hawajawahi kuwa na dhamira ya kweli kuhusu haki za binadamu za wananchi wa Iran; la sivyo, wasingekuwa wameweka vikwazo visivyo vya kibinadamu vinavyokiuka haki za msingi za kila Muirani, wala wasingeliunga mkono mashambulizi ya kijeshi ya utawala wa Israel mwezi Juni yaliyosababisha kuuawa kwa Wairani wasio na hatia.
Alieleza kwamba Iran ina mifumo yake huru ya kitaifa ya kuchunguza na kuhakikisha uwajibikaji kuhusiana na vitendo vya vurugu na ugaidi vilivyojitokeza wakati wa machafuko ya hivi karibuni yaliyoungwa mkono na tawala za kigeni.
Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesisitiza kuwa hadhi ya kisheria ya kila mfungwa itachunguzwa kwa mujibu wa sheria za nchi, akibainisha kuwa wale watakaothibitika kuwa na hatia watakabiliwa na uwajibikaji kamili wa kisheria kupitia mchakato wa kesi ulio wa haki, usio na upendeleo, na ulio wazi kwa mujibu wa viwango vya kimataifa.
Bahreini aliongeza kwamba: “Ingawa Iran haitaki kuanzisha vita, iko tayari kikamilifu kulilinda taifa lake, ardhi yake, na uhuru wake dhidi ya tishio lolote, kwa kiwango chochote, kutoka chanzo chochote.”
Siku ya Jumatano Taasisi ya Mashahidi ya Iran iliripoti kwamba watu 3,117 walipoteza maisha wakati wa machafuko hayo, wakiwemo raia na maafisa wa usalama 2,427, ikibainisha kuwa watu wengi wasio na hatia waliuawa shahidi katika mashambulizi makundi ya kigaidi yaliyojipanga.
Kwa mujibu wa taarifa ya Baraza la Usalama la Iran, kilele cha ukatili kilijitokeza tarehe 8 na 9 Januari, wakati washambuliaji walipotekeleza “uhalifu wa mtindo wa Daesh,” ikiwemo kukatakata watu, kuwachoma wakiwa hai, na mashambulizi ya visu. Hayo yaliambatana na mashambulizi ya kimfumo dhidi ya masoko, maduka, benki, misikiti, hospitali, magari ya wagonjwa na miundombinu mingine ya umma.