
Uchunguzi mpya wa maoni umebaini kwamba katika baadhi ya nchi kubwa barani Ulaya, watu wengi zaidi wanamwona rais wa Marekani kama “adui” kuliko “rafiki” au mshirika wa Ulaya.
Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa leo na jarida la masuala ya jiopolitiki Le Grand Continent, walio wengi Ulaya wanamwona Donald Trump kama “adui wa Ulaya” kufuatia vitisho vyake vya kutaka kulinyakua kwa nguvu eneo la Greenland, ambalo ni eneo lenye mamlaka ya ndani la Denmark na utajiri mkubwa wa madini.
Uchunguzi huo unaashiria kwamba vitisho vya Trump dhidi ya Greenland vimewageuza raia wengi wa Ulaya kuwa dhidi ya Marekani.
Mahojiano yaliyofanywa na zaidi ya watu 7,000 katika nchi saba za Ulaya—Ujerumani, Ufaransa, Italia, Poland, Uhispania, Denmark na Ubelgiji—kati ya Januari 13 na 19, yalionyesha kuwa asilimia 51 walimwona Trump kama “adui,” asilimia 8 tu ndio waliomwona kama “rafiki,” na takribani asilimia 39 walimwona kama “si rafiki wala adui.”
Hata hivyo, idadi kubwa, asilimia 81 ya watu wa Ulaya, wanaamini kwamba hatua ya Trump ya kutaka kulinyakua eneo la Greenland kwa nguvu za kijeshi inapaswa kuchukuliwa kama “kitendo cha kivita dhidi ya Ulaya.”
Aidha, takribani asilimia 63 ya waliohojiwa walisema wanaunga mkono kutumwa kwa wanajeshi wa Ulaya kwenda katika kisiwa hicho ili kukilinda dhidi ya uwezekano wa uvamizi wa Marekani.
Hususan, wananchi wa Denmark walikuwa miongoni mwa waliomwona Trump kama “adui wa Ulaya,” ambapo asilimia 58 ya waliohojiwa nchini humo walitoa mtazamo huo.
Baadhi ya viongozi wa Ulaya wamependekeza kuwa wanaunga mkono matumizi ya nguvu dhidi ya Marekani, kwani wanauchukulia mwenendo wa Trump kuwa wa uporaji na wa kutaka kutawala kwa mabavu.
Viongozi wa Ulaya wamekubaliana kutuma wanajeshi kutoka bara hilo ili kuilinda Greenland dhidi ya uwezekano wa uvamizi wa Marekani.
Trump anasisitiza kwamba Marekani “inahitaji” kuimiliki Greenland kwa sababu za kiusalama. Hata hivyo, wakosoaji wake wanasema ukweli ni kwamba analenga kupata “umiliki kamili” wa rasilimali za madini ambazo bado hazijachimbuliwa katika Greenland, kabla mataifa mengine hayajapata nafasi.