
Bangladesh imesema “imeshangazwa” na “kushtushwa” kuona India imemruhusu waziri mkuu wa zamani mtoro Sheikh Hasina kutoa hotuba ya hadhara mjini New Delhi.
Hasina, mwenye umri wa miaka 78, alikimbilia nchi jirani ya India Agosti 2024 baada ya uasi wa umma ulioongozwa na wanafunzi uliohitimisha utawala wake wa miaka 15 wa kuitawala Bangladesh kwa mkono wa chuma.
Mwanasiasa huyo alitoa hotuba yake hiyo ya kwanza ya hadhara siku ya Ijumaa kwa njia ya sauti alipohutubia klabu ya waandishi wa habari iliyojaa wanahabari mjini Delhi.
Hasina alipatikana na hatia ya makosa ya uchochezi, kutoa amri ya kuua na kutochukua hatua za kuzuia vitendo vya ukatili na hivyo kuhukumiwa kifo na mahakama ya Dhaka mnamo Novemba mwaka jana bila yeye mwenyewe kuwepo mahakamani.
“Serikali na watu wa Bangladesh wameshangazwa na kushtushwa,” imeeleza taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo.
“Kuruhusu tukio hilo kufanyika katika mji mkuu wa India na kumruhusu muuaji wa halaiki Hasina kutoa hotuba yake ya chuki waziwazi ni aibu dhahiri kwa watu na Serikali ya Bangladesh”, imesisitiza taarifa hiyo.
Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Bangladesh imebainisha kuwa kumruhusu Hasina kutoa hotuba hiyo kunaanzisha “mfano hatari” ambao unaweza “kuharibu vibaya sana uhusiano wa pande mbili”.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, wapiga kura nchini Bangladesh wataelekea vituo vya kupigia kura Februari 12 kuchagua viongozi wapya baada ya kipindi cha machafuko yaliyofuatiwa na kupinduliwa serikali ya Bi. Hasina.
Hasina alisema katika hotuba yake aliyotoa kwa njia ya sauti kwamba “Bangladesh haitawahi katu kuwa na uchaguzi huru na wa haki” chini ya kiongozi wa mpito Muhammad Yunus.
Zaidi ya watu 100,000 waliisikiliza hotuba hiyo, ambayo ilirushwa mtandaoni.
Bangladesh imeiomba India imrejeshe Hasina nchini humo, lakini New Delhi bado haijatoa maoni yoyote kuhusiana na ombi hilo.
Uungaji mkono wa India kwa Hasina tangu enzi za utawala wake umeharibu uhusiano wa majirani hao wa Asia Kusini tangu yeye alipong’olewa madarakani…/