
Uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa Wajerumani wengi wanamtambua Rais wa Marekani, Donald Trump, kama tishio kwa nchi yao.
Uchunguzi huo wa maoni uliyofanywa na taasisi ya INSA ya Vipimo vya Maoni kwa niaba ya gazeti la Ujerumani la Bild am Sonntag na kuchapishwa leo, Jumapili, ambao umeshirikisha watu wapatao elfu moja, umeonyesha kuwa 61% ya waliohojiwa wanamuona Trump kama hatari na tishio kwa Ujerumani.
Kwa upande mwingine, 24% ya washiriki wanamuona rais wa Marekani kama mshirika wa nchi yao, huku 15% wakikataa kutoa maoni.
Wengi kati ya washiriki katika uchunguzi huo wa maoni wanaamini kwamba serikali ya Ujerumani inapaswa kutumia mbinu kali zaidi katika kukabiliana na rais wa Marekani. 52% ya waliohojiwa wameunga mkono suala la kuchukua msimamo mkali zaidi dhidi ya sera zake, huku 31% wakiona kupanua ushirikiano na kiongozi huyo kama chaguo linalofaa zaidi.
Utafiti huo ulifanyika kati ya Januari 22 na 23.
Ukosoaji wa Ulaya dhidi ya mienendo ya utawala wa Marekani umeongezeka hivi karibuni, hasa baada ya mzozo wa Greenland, wakati rais wa nchi hiyo, Donald Trump alipoitishia Denmark kwa vita vya kibiashara na hatua za kijeshi ikiwa haitaikabidhi eneo la Greenland.
Awali, chunguzi mpya wa maoni ulibaini kwamba katika baadhi ya nchi kubwa barani Ulaya, watu wengi zaidi wanamwona rais wa Marekani kama “adui” kuliko “rafiki” au mshirika wa Ulaya.
Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa jana na jarida la masuala ya jiopolitiki Le Grand Continent, walio wengi Ulaya wanamwona Donald Trump kama “adui wa Ulaya” kufuatia vitisho vyake vya kutaka kulinyakua kwa nguvu eneo la Greenland, ambalo ni eneo lenye mamlaka ya ndani la Denmark na lenye utajiri mkubwa wa madini.
Viongozi wa Ulaya wamekubaliana kutuma wanajeshi kutoka bara hilo ili kuilinda Greenland dhidi ya uwezekano wa uvamizi wa Marekani.