Makaburi mawili ya umati yenye mabaki ya miili ya maelfu ya watu yalipatikana hivi majuzi mjini Khartoum mji mkuu wa Sudan. Kupatikana kwa makaburi hayo kumefichua sura ya giza katika mzozo unaoendelea Sudan kati ya jeshi la taifa na wanamgambo wa kundi la Rapid Support Forces (RSF)

Duru za ndani ya Sudan zimeeleza kuwa makaburi mawili ya umati yamegunduliwa katika kitongoji cha Riyadh karibu na mtaa wa Obeid Khatim huko Khartoum. Mabaki ya miili yaliyopatikana ndani yamakaburi hayo mawili ya umati yameonyesha kuwa wahanga walizikwa kwa njia isiyo ya kawaida.

Duru hizo zimeeleza kuwa wanamgambo wa RFS walitumia majengo ya karibu na kitongoji cha Riyadh ambayo awali yalitumiwa na kituo cha uongozi cha RSF kama vituo vya kuwashikilia watu na kama jela..

Wakati huo huo watu walioshuhudia wameeleza kuwa raia na wanajeshi walioaga dunia kwa kuteswa katika jela za wanamgambo wa RSF walisafirishwa na wafungwa wenzao na kuzikwa kwenye mashimo yaliyochimbwa kwa kutumia mashine nzito.

Idadi kubwa ya ndala na viatu, pamoja na vifaa mbalimbali vya watu vinaweza kuonekana karibu na makaburi hayo ya umati jambo linalodhihirisha ukubwa wa maafa yaliyotokea katika kitongoji cha Riyadh katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum. 

Intisar Ahmed Abdel Mutaal Mwendesha Mashtaka  wa Sudan amesema kuwa: “Idadi kubwa ya wahanga imechelewesha kufukuliwa makaburi hayo ya umati. Jitihada zinafanywa ili kufukua makaburi hayo na kuhamishia miili katika makaburi sahihi. Idadi ya waliozikwa ni kubwa sana, na kuna miili ambayo ilizikwa shuleni, katika vyuo vikuu na maeneo ya umma.”

“Zoezi la kufukua makaburi linafanywa kwa uratibu wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), na miongoni mwa changamoto  zilizopo ni ukosefu wa rasilimali na idadi kubwa ya miili,” amesema Mwendesha Mashtaka wa Sudan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *