
Jeshi la Mali (FAMa) limetangaza kuwa limewaua zaidi ya magaidi 100 katika mashambulizi ya anga liliyofanya kwenye eneo la msitu katikati mwa nchi siku ya Jumapili, na kuyataja mashambulio hayo kuwa ni operesheni muhimu dhidi ya magaidi katika eneo hilo.
Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo siku ya Jumatatu imeeleza kwamba wakati wa mashambulizi ya angani Januari 25, “walishambulia kwa ufanisi kutoka angani” kambi ya makundi ya magaidi. Eneo hilo lilikuwa katika msitu wa Soussan, magharibi mwa Dioila na kusini magharibi mwa Zantiguila.
“Wamesema idadi ni zaidi ya magaidi 100 ambao walikatwa makali, pamoja na silaha kuteketezwa” imesisitiza taarifa hiyo ya FAMa.
Mali imekabiliwa na changamoto ya usalama tangu mwaka 2012, sambamba na kukumbwa na mashambulizi ya magaidi, hasa katika maeneo ya kaskazini na katikati.
Makundi hayo ya magaidi yameshtumiwa kwa kuzuia mafuta kuingia nchini humo katika miezi ya hivi karibuni.
Makundi hayo ya kigaidi yalishadidisha mashambulizi ya kulipiza kisasi baada ya mamlaka kupiga marufuku uuzaji wa mafuta nje ya vituo rasmi katika maeneo ya vijijini, hatua iliyolenga kutatiza magaidi hao kupata mafuta…/