
Mataifa kadhaa ya Kiislamu na Kiarabu yameulaani vikali utawala haramu wa Israel kwa kukiuka usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza
Katika radiamali yao kwa mvutano unaoendelea katika Ukanda wa Gaza, nchi nane za Kiarabu na Kiislamu zimetoa taarifa ya pamoja ya kuonya kuhusu matokeo hatari ya vitendo vya utawala wa Israel na athari zake kwenye mchakato wa kisiasa na utulivu wa eneo hilo.
Kanali ya Televisheni ya Al Jazeera ya Qatar imeripoti kwamba, nchi nane za Kiarabu na Kiislamu zimelaani vikali katika taarifa ya pamoja, ukiukwaji wa mara kwa mara wa makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza na utawala wa Israel, na kuvitaja vitendo hivyo kama tishio kubwa kwa amani na utulivu katika eneo hilo.
Taarifa hiyo inasema kwamba, vitendo vya utawala wa Kizayuni vinaweza kusababisha kuongezeka mivutano na kudhoofisha juhudi za kuanzisha amani na kurejesha utulivu wa kudumu.
Kwa mujibu wa al-Jazeera nchi za Misri, Jordan, Umoja wa Falme za Kiarabu, Indonesia, Pakistani, Uturuki, Saudi Arabia na Qatar zimezihimiza pande zote kutekeleza majukumu yao kikamilifu katika hatua hii muhimu na kuchukua hatua ya kujizuia ili kuhakikisha udumishaji na mwendelezo wa usitishaji mapigano.
Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi hizo wamesisitiza tena umuhimu wa kufikia amani ya haki, kamili, na ya kudumu, na wakatangaza kwamba, amani hii lazima itegemee haki isiyoweza kuondolewa ya watu wa Palestina ya kujitawala na kuanzishwa taifa lao huru, kwa kuzingatia sheria za kimataifa, maazimio husika ya Baraza la Usalama, na Mpango wa Amani wa Kiarabu.