16 Bora Ligi ya Mabingwa Ulaya kuanza leo na rekodi tofauti16 Bora Ligi ya Mabingwa Ulaya kuanza leo na rekodi tofauti

Hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya inaanza leo Jumanne, Machi 10, 2026, ambapo timu nane zitaumana katika viwanja na miji minne tofauti barani Ulaya kusaka tiketi za kucheza hatua ya robo fainali.

Liverpool itakuwa ugenini katika Uwanja wa Rama Park, Istanbul Uturuki kukabiliana na wenyeji wao, Galatasaray.

Hii ni mara ya pili kwa timu hizo kukutana msimu huu ambapo katika mechi ya kwanza ambayo ilikuwa ya hatua ya Ligi, Liverpool ilipoteza kwa bao 1-0.

Nyota wa Liverpool, Florian Wirtz, akiwashukuru mashabiki wa timu hiyo baada ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kumalizika kwa kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Galatasaray katika hatua ya ligi msimu huu. Picha na Mtandao

Newcastle United itakuwa katika Uwanja wake wa nyumbani wa St. James’ Park kuikaribisha Barcelona.

Barcelona inaingia katika mchezo huo ikiwa na rekodi nzuri dhidi ya timu za England katika hatua za mtoano za Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo tangu 2014, imepata ushindi mara 10 katika mechi 12.

Atalanta itakuwa nyumbani katika Uwanja wa New Balance kuikaribisha Bayern Munich ikiwa na rekodi mbaya ya kupoteza mechi sita kati ya saba zilizopita za hatua ya mtoano.

Baadhi ya wachezaji wa kikosi cha Bayern Munich wakiwa katika Uwanja wa mazoezi kabla ya pambano la Ligi ya Mabingwa Ulaya litakaloikutanisha dhidi ya Atalanta Bergamo. Picha na Mtandao

Bayern Munich itacheza huku ikijivunia rekodi nzuri ya kupoteza mechi moja tu kati ya 16 zilizopita za hatua ya mtoano.

Mchezo mwingine leo utakuwa baina ya Atletico Madrid na Tottenham Hotspur ambao utachezwa katika Uwanja wa Metropolitano.

Wenyeji Atletico Madrid wanaingia katika mchezo huo wakiwa na rekodi nzuri ya kutopoteza mechi nyumbani katika hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *