Watu wasiopungua 26 wameuawa katika mashambulizi matatu tofauti mwishoni mwa wiki ya Pasaka kaskazini mwa Nigeria, kulingana na jeshi la Nigeria na mamlaka za ndani.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Angalau watu 17 waliuawa siku ya Jumamosi wakati watu wenye bunduki waliposhambulia jamii ya Mbalom katika eneo la Gwer Magharibi mwa Jimbo la Benue, kaskazini-katikati mwa Nigeria.

Gavana wa Jimbo la Benue, Hyacinth Alia, alithibitisha mashambulizi hayo siku ya Jumapili, lakini hakutaja idadi ya waathiriwa. Wakazi waliripoti 17.

Mashambulizi kama hayo ni sehemu ya mzunguko wa muda mrefu wa vurugu kaskazini-katikati mwa Nigeria, ambapo migogoro kuhusu ardhi na haki za malisho kati ya wafugaji wengi wao wakiwa Waislamu wa Fulani na jamii nyingi za wakulima Wakristo mara nyingi huongezeka na kuwa makabiliano makali. Magenge ya wahalifu pia yanaendesha uhalifu wao.

Tarhana Samson, mkazi wa jamii hiyo, alielezea mashambulizi hayo kama “mabaya sana.”

“Msimu wa mvua unakaribia, na huu ndio wakati ambapo watu hujiandaa kwenda mashambani. Watawezaje sasa?” Bw. Samson alijiuliza.

Katika shambulio jingine mapema Jumamosi asubuhi kwenye makao makuu ya polisi katika Jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa nchi, maafisa wanne wa polisi waliuawa baada ya mapigano marefu ya kurushiana risasi na kundi linalohusiana na ISIS, kulingana na Kenneth Daso, afisa wa uhusiano wa umma wa polisi wa Borno.

Siku ya Jumapili, wakati wa ibada ya Pasaka katika kijiji cha Ariko, katika Jimbo la Kaduna, watu wenye silaha waliwaua watu watano, kulingana na jeshi.

Utambulisho wa watu hao wenye silaha haujulikani. Jeshi lilisema kwamba washambuliaji walilazimika kuachana na utekaji nyara wa mateka 31 baada ya wanajeshi kuitikia wito wa dharura.

“Kwa bahati mbaya, miili ya waathiriwa watano ambao wliuawa na magaidi hao pia ilipatikana katika eneo la tukio,” jeshi lilisema. “Magaidi hao waliotimka baada ya jeshi kuingilia kati, wanaaminika kupata hasara kubwa, kama inavyothibitishwa na madoa ya damu kando ya barabara walizotumia kwa kutoroka.”

Kaduna inaendelea kukumbwa na mashambulizi dhidi ya makanisa na utekaji nyara wa mara kwa mara. Mnamo mwezi Januari, zaidi ya waumini 150 walitekwa nyara huko Kurmin Wali, kijiji ambacho kinapatikana katika mkoa wa Kajuru huko Kaduna, takriban kilomita 60 kutoka eneo la shambulio la Jumapili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *