Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imeanza kutekeleza mradi wa kusambaza majiko banifu zaidi ya 10, 300 kwa Wananchi mkoani Tabora.
Mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ikiwamo lengo la asilimia 80 ya Watanzania wanatumia Nishati Safi ya kupikia ifikapo 2034.
Akizungumza leo Jumamosi, Aprili 11,2026 wakati wa kutambulisha mtoa huduma, Kampuni ya Burn manufacturing Tanzania Ltd. aliyeshinda zabuni ya kusambaza majiko hayo kwa Mkoa wa Tabora, Mhandisi Miradi kutoka REA, Ramadhan Mganga amesema Serikali kupitia REA imetoa Sh 641,291,596 kwa ajili ya ruzuku ya majiko hayo kwa Mkoa huo.
“Dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuendelea kuboresha maisha ya wananchi pamoja na kulinda mazingira kwa kuhakikisha nishati safi za kupikia zinapatikana kwa bei nafuu zaidi na ndio maana akaridhia kutoa fedha kama ruzuku katika majiko hayo.”
“Majiko hayo kwa bei ya kawaida ni Sh62,000 mpaka Sh 70,000 lakini baada ya Serikali kuweka ruzuku ya asilimia 80 sasa mwananchi atalipia Sh12,500 peke kupata jiko hili na kiasi kilichobaki Serikali inalipia,” amesema Mhandisi Mganga.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, CPA. Amos Ackim amesema wamejipanga pamoja na watendaji katika wilaya zote sita za mkoa huo zitakazonufaika na mradi huo kuhakikisha wananchi waliokusudiwa wanafikiwa na malengo ya mradi huo yanafikiwa.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Mohamed Mtulyakwaku amewahamasisha wananchi kuendelea kuunga mkono kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kununua majiko banifu ambayo ni rafiki kwa mazingira na ni rafiki pia kwa afya ya anayetumia.
(Feed generated with FetchRSS)