Wasichana wa shule ya Sekondari Songwe iliyopo Wilaya ya Momba Mkoani Songwe wameanza kufanya vizuri katika masomo ya sayansi baada ya kupata maabara na kuimarika kwa mazingira ya kujifunzia hali iliyoongeza ari na hamasa ya kupenda masomo hayo.

Sifael Mboma (15), mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule hiyo anaona sayansi siyo tu masomo ya darasani bali ni sehemu ya maisha ya kila siku. Anazungumzia masomo ya sayansi kwa msisimko na kujiamini akieleza namna yanavyomvutia na kumpa mwelekeo wa maisha yake ya baadaye.

“Ukiangalia maisha yetu ya kila siku yamezungukwa na sayansi kama vile uhandisi. Tunaishi katika nyumba na majengo yaliyojengwa kwa utaalamu huo,” anasema kwa msisitizo.

Sifael anasema, sayansi ni daraja la suluhu za changamoto katika jamii. Anaamini kuwa kujikita katika taaluma hizo kutasaidia kuongeza idadi ya wataalamu wa kike katika sekta muhimu kama uhandisi na udaktari.
“Wanawake wanapopata huduma kutoka kwa wataalamu wenzao, wanakuwa huru na kupata faraja zaidi,” anasema.

Sifael pia ana ujumbe mzito kwa wasichana wenzake kuwa waachane na hofu na dhana potofu kwamba masomo ya sayansi ni magumu au ni ya wavulana pekee.
Hadithi ya Sifael si ya kipekee bali ni sehemu ya wimbi jipya la wasichana mkoani Songwe wanaoanza kuonyesha uthubutu katika masomo ya sayansi.

Katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Songwe, mafanikio yanaonekana wazi. Mkuu wa shule hiyo Janeth Mwamwile anasema kati ya wanafunzi 25 waliohitimu kidato cha nne mwaka 2025, 12 walipata daraja la kwanza, wanne daraja la pili, wanane daraja la tatu, mmoja daraja la nne na hakuna aliyepata daraja sifuri ishara ya mabadiliko chanya yanayochipuka.

Katika wilaya jirani ya Mbozi, simulizi kama hiyo inaendelea kujitokeza. Judith Mgode mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Ndugu na Edna Rajab wa kidato cha tatu kutoka Shule ya Sekondari Shiwinga, ni miongoni mwa wasichana wanaothibitisha kuwa uwezo wa kufaulu masomo ya sayansi hauchagui jinsia. Judith anasisitiza kuwa mafanikio yanahitaji bidii na nidhamu, bila kujali somo analosoma mwanafunzi.

#StarTvUpdatz

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *