Dar es Salaam. Filamu ya wasifu wa marehemu Mfalme wa Pop kutoka Marekani, Michael Jackson, imeibua mjadala baada ya wadau na wachambuzi wa burudani kudai itaonyesha maisha ya msanii huyo kwa upande mmoja.
Kwa mujibu wa gazeti la The Daily Telegraph, wameripoti wakieleza filamu hiyo imeelezea tu safari yake na maisha yake ya kimuziki kwa ujumla huku wakiacha kugusia tuhuma za unyanyasaji zilizowahi kumkabili, jambo ambalo linadaiwa kuwa imekuja kusafisha jina la MJ. Huku wakisisitiza filamu hiyo imezingatia zaidi biashara kuliko uhalisia.
Ripoti ya Variety inaeleza kuwa baadhi ya vipande vilivyogusia tuhuma hizo viliondolewa kutokana na masharti ya kisheria yaliyokataza kutajwa kwa Jordan Chandler kwenye jambo lolote linalomuhusisha MJ. Hivyo, filamu hiyo inadaiwa kuishia miaka ya 1980 kabla ya kashfa kuanza.
Ikumbukwe Mwaka 1993, kijana mmoja ambaye alikuwa na umri wa miaka 13, Jordan Chandler, alimshutumu Jackson kwa unyanyasaji wa kingono. Kesi hiyo haikufikishwa mahakamani na badala yake ilimalizika kwa makubaliano ya kifedha (settlement) nje ya mahakama. Jackson hakukiri kosa lolote, lakini tukio hilo liliharibu kwa kiasi kikubwa taswira yake mbele ya umma.
Michael Jackson akiwa na mpwa wake Jaafar Jackson ambaye ndiye amevaa uhusika kwenye filamu hiyo ya MJ
Vilevile mwaka 2005 alifikishwa mahakamani akishtakiwa kwa tuhuma za unyanyasaji dhidi ya kijana mwingine aliyekuwa na umri wa miaka 13. Baada ya kesi kubwa iliyokuwa kifuatiliwa kwa shauku, baraza la majaji lilimkuta hana hatia kisha kesi hiyo kufungwa kabisa.
Mbali na kuficha kuhusu kesi za unyanyasaji wa kingono lakini pia, baadhi ya wadau wa burudani wanaeleza kuwa jambo lingine lililofichwa ni MJ kuhusishwa na kujichubua pamoja na kubadilisha mwonekano wake.
Ambapo mpwa wake Jaafar Jackson wakati alipokuwa kwenye mahojiano na waandishi wa habari alimtete mjomba wake ambaye alidaiwa kubadilisha mwonekano wake ili afanane na watu wenye ngozi nyeupe ‘Mzungu’.
“Dhana potofu kubwa ni kwamba alitaka kuwa mzungu. Huo ni uongo mkubwa, na filamu hii inakupa uelewa wa hilo kwamba ugonjwa wa ngozi unaoitwa vitiligo ulikuwa na mchango mkubwa katika maisha yake. Watu wengi hawalielewi jambo hilo. Alikuwa akipambana na hali hiyo tangu akiwa mdogo,”alisema Jaafar
Vitiligo ni hali ya kiafya inayosababisha ngozi kupoteza rangi au pigmenti. Kwa mujibu wa The Vitiligo Clinic and Research Center at UMass Chan Medical School, ripoti ya uchunguzi wa mwili (autopsy) ya Michael Jackson ilibaini kuwepo kwa “madoa yenye rangi nyepesi na nyeusi” kwenye ngozi yake wakati wa uchunguzi. Pia, vitiligo iliorodheshwa kama mojawapo ya magonjwa katika historia yake ya kiafya.
Taasisi hiyo pia ilieleza kuwa mshindi huyo wa tuzo za Grammy alitumia krimu iitwayo Benoquin 20%, ambayo ni tiba iliyoidhinishwa na U.S. Food and Drug Administration kwa ajili ya matibabu ya vitiligo.
Mbali na hiyo alitumia pia aina nyingine ya matibabu ya hali hiyo, na kumsababishia ugonjwa uliyopelekea ngozi kupoteza rangi yake ya asili na kuwa nyeupe.
MJ ambaye amewahi kutamba na wimbo kama Thriller, alifariki dunia Juni 25, 2009 akiwa na umri wa miaka 50, huko Los Angeles, Marekani. Filamu inayoelezea maisha yake iliyopewa jina la Michael bado haijatoka, inatarajiwa kuanza kuoneshwa katika kumbi za sinema duniani kote Ijumaa Aprili 24, 2026.