
SINGIDA Black Stars imeshaanza maisha jijini Dar es Salaam baada ya kuondolewa mapema kwenye mashindano ya Kombe la Mashndano na wakati inalia na mwamuzi inayedai aliwaharibia, lakini wasi-isahau Azam FC.
Iko hivi; Singida ilitolewa na Mlandege ikikubali kichapo cha mabao 2-1 kwenye mchezo wa robo fainali, tena ikitoka kuongoza bao 1-0 na kugeuziwa kibao ikichapwa.
Inachotakiwa kufahamu Singida ni kwamba, mchawi wao ndani ya matokeo hayo ni mastaa wanne wa Azam FC ambao wako ndani ya Mlandege ambao waliifanya kazi kubwa ya kutengeneza matokeo hayo.
Ndani ya ukuta wa Mlandege, kitasa cha kati beki Vellim Opondo ambaye aliwazima washambuliaji wa timu hiyo ni mali ya Azam FC ambaye anaitumikia timu hiyo kwa mkopo.
Opondo ambaye anapenda kuitwa Yondani, akihusudu kucheza kama mkongwe Kelvin Yondani, kwenye mchezo huo alikuwa mwiba mkali kwa Singida akitibua hesabu nyingi za washambuliaji wa Sin-gida.
Achana na Opondo, pale kati kulikuwa na viungo wawili mafundi Jamal Saleh maarufu kwa jina la Jaku, jamaa anajua kupiga pasi akitumia mguu wa kushoto ambapo alikuwa kila akishika mpira ana balaa.
Mwingine ni Mahmoud Haji ambaye naye alikuwa eneo hilo la kati akifanya kazi kubwa ya kukaba kwa nguvu na kuanzisha mashambulizi ambapo pasi yake moja ya mwisho ilizalisha bao la pili kwa Mlandege. Viungo hao wawili wote ni mali ya Azam FC wakiitumikia Mlandege kwa mkopo wakionye-sha ubora mkubwa kwenye mchezo huo ambao ulikuwa mkali ndani ya dakika zote 90. Kule mbele sasa kulikuwa na washambuliaji wawili, wa kwanza ni Omar Juma ‘Sammata’ aliyefunga bao la kwanza kwa ufundi kwenye mchezo huo akiisawazishia timu yake iliyokuwa nyuma kwa bao 1-0 na kufaya mchezo kuwa 1-1 akiirudisha Mlandege mchezoni, jamaa ni mali ya Azam FC. Mwingine ni Mussa Hassan ‘Mbappe’ ambaye aliifungia Mlandege bao la pili kwenye mchezo huo naye ni mali ya Azam FC akicheza hapo kwa mkopo ambapo mastaa hao wanne ni silaha nzito zilizotoka kwa matajiri hao wa Chamazi.