BAADA ya Raja Casablanca ya Morocco, kuhusishwa kutaka huduma ya beki wa kati wa Yanga, Ibrahim Abdallah Hamad ‘Bacca’, kuna staa mwingine wa Ligi Kuu Bara anatakiwa na klabu hiyo.
Taarifa mpya zinahusiana na klabu hiyo, kuhitaji huduma ya kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ikitajwa ni mapendekezo ya kocha Fadlu Davids aliyewahi kuifundisha Simba msimu wa 2024-2025 na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Chanzo hicho kilisema wachezaji hao wawili wapo katika rada ya Raja, hivyo kinachoangaliwa kwa sasa ni masharti ya mikataba yao kama inawezekana kuvunjwa ama kununuliwa.
Kabla ya taarifa ya Fei Toto kutakiwa na Raja, Mwanaspoti liliandika kuhusiana na Bacca huduma yake kutakiwa na klabu hiyo na masharti ya kumpata yalielezwa.
Bacca ni askari wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) akiwa na cheo cha sajenti, hivyo uongozi kupitia kwa Capteni (N) Hussein Ali Makame ambaye ni mkuu wa teknolojia na michezo, alitaja masharti ya usajili wa staa huyo endapo kama atahitajika na klabu nyingine nje na Yanga anayoitumikia kwa sasa.
Capteni Makame alisema: “Kama kweli ishu hiyo ipo, Bacca na uongozi wa Yanga watatujulisha, ila hadi sasa hatuna taarifa yoyote kuhusiana na Bacca kutakiwa na Raja.”
Aliongeza: “Askari yeyote kutoka KMKM iwe mchezaji ama kazi nyingine, mfano baharia akipata dili la kampuni za nje anaruhusiwa kwenda lakini ile kampuni itatambua sisi ndiyo waajiri wake na lazima tutapata pesa kiasi kutoka kwao, tunaamini kwa kufanya hivyo tunawaongezea ujuzi na uzoefu mwingine.”
Kuhusiana na taarifa za Fei Toto, chanzo hicho kilisema: “Siyo mara ya kwanza kwa Raja kumtaka Fei Toto, tunarejea kwake kwa mara nyingine tena.”
Mwanaspoti lilimtafuta Fadlu ili kujua taarifa hizo zina ukweli gani ambapo Msauzi huyo alijibu anaweza akawazungumzia kile wanachokifanya uwanjani, lakini siyo usajili kwani hao ni wachezaji wa timu nyingine.
“Nawakubali ni wachezaji wazuri na wenye uwezo wa hali ya juu uwanjani na wana muendelezo wa viwango vyao, lakini siwezi kuzungumza vinginevyo kwani ni wachezaji wa klabu zingine na wana mika-taba na timu hizo,” alisema Fadlu.
FEI TOTO NA AZAM
Huu ni msimu wa tatu Fei Toto anaitumikia Azam aliyojiunga nayo 2023-2024 akitokea Yanga, huku aki-wa mchezaji mwenye mchango mkubwa kikosi hapo kiasi cha kuzivutia klabu mbalimbali.
Wakati wa mkataba wake ukielekea ukingoni, Fei Toto tayari ameongeza mwingine unaomfanya ku-salia Azam hadi mwaka 2027, hivyo kama kuna timu inamuhitaji haina budi kuuvunja.
Kabla ya kuongeza mkataba huo ambao maslahi yake yameboreshwa ikiwemo mshahara ulioripotiwa ni zaidi ya Sh50 milioni, nyumba ya kuishi na ada ya usajili takribani Sh800 milioni sambamba na gari ya kutembelea, kiungo huyo anayeongoza kwa asisti Ligi Kuu Bara akiwa nazo saba huku pia akifunga mabao saba, alikuwa akiwindwa na klabu za ndani na nje ya Tanzania.
Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ilionyesha nia ya dhati ya kumsajili kiungo huyo tangu dirisha la usajili la Januari 2026.
Nyingine ni Al-Ittihad ya Libya iliripotiwa kuwa tayari kutoa dau la Dola milioni 2.5 (takriban Sh6.5 bilioni) ili kumnasa Fei Toto mwishoni mwa mwaka 2025. Pia zilikuwepo MC Alger ya Algeria na Pyramids FC ya Misri. Mbali na klabu hizo za nje, Yanga na Simba pia zilitajwa kumfuatilia kwa karibu, huku kukiwa na tetesi za yeye kurejea Yanga kuchukua nafasi ya Stephane Aziz Ki aliyeondoka mwishoni mwa msimu uliopita 2024-2025.
Azam inamchukulia Fei Toto kama nguzo muhimu katika mipango yao ya kutwaa ubingwa wa ligi na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa msimu ujao baada ya msimu huu kuweka rekodi ya ku-cheza hatua ya makundi kwa mara ya kwanza kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, huku timu hiyo sasa ikiwa nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 37, nyuma ya Simba (42) na vinara Yanga (47).