KOCHA Mkuu wa Fountain Gate, Fred Felix ‘Minziro’ amesema ushindi walioupata kwenye mchezo uliopita katika Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar, umeongeza morali kwa wachezaji wake, huku akisisitiza kuwa maandalizi kuelekea mchezo ujao yanaendelea kwa umakini mkubwa.

Hata hivyo, Minziro ameweka wazi kuwa, benchi la ufundi limejikita kuboresha maeneo matatu muhimu ambayo yatawasaidia kuwa bora zaidi kwenye mechi zijazo, lengo likiwa ni kuiweka salama timu hiyo isishuke daraja.

Kocha huyo ambaye amekabidhiwa jukumu la kuiongoza Fountain baada ya kuondoka Mohamed Ismail ‘Laizer’, tayari amesimamia mechi mbili za ligi akianza na kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Simba, kisha ushindi wa 2-1 mbele ya Mtibwa Sugar.

“Ushindi ule umetupa hamasa kubwa, lakini bado tuna mambo ya kuboresha,” amesema Minziro, kocha aliyewahi kufundisha timu kadhaa za Ligi Kuu Bara ikiwemo Yanga na Pamba Jiji.

“Eneo la kwanza ni umakini kwenye umaliziaji wa nafasi, wachezaji wamekuwa wakitengeneza nafasi nyingi lakini wanahitaji kuwa makini zaidi kuzitumia.

“Jambo la pili tunafanyia kazi uimara wa safu ya ulinzi ili kuepuka makosa yanayoweza kutugharimu kwenye michezo migumu.

“Pia tumeweka mkazo kwenye kuongeza pumzi na stamina kwa wachezaji wote ili waweze kuhimili kasi ya mchezo kwa dakika zote 90.”

Akizungumzia mchezo ujao dhidi ya Pamba Jiji utakaochezwa Aprili 30 mwaka huu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Minziro amesema hautakuwa rahisi kutokana na ubora wa wapinzani wao ambao wamewazidi pointi.

“Huu ni mchezo mgumu, tunawaheshimu Pamba, lakini sisi tupo tayari kupambana kuhakikisha tunapata ushindi,” amesema.

Fountain Gate itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na rekodi ya matokeo mazuri dhidi ya Mtibwa Sugar na kujiimarisha zaidi kwenye msimamo wa ligi ambapo ina pointi 19 sawa na mechi ilizocheza ikikamata nafasi ya 13.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *