
Dar es Salaam. Hakuna kukata tamaa, ndivyo ilivyokuwa kwa baadhi ya wanasiasa waliowania ubunge kupitia CCM, lakini majina yao kukatwa, sasa wameibukia ubunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Eala).
Hatua hiyo inaashiria wanasiasa hao kuamua kutafuta njia mbadala ya kuendelea na shughuli za uwakilishi wa wananchi katika ngazi ya kikanda.
Miongoni mwao wamo waliowahi kushika nyadhifa za juu serikalini, wakiwemo waliowahi kuwa naibu mawaziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa nyakati tofauti.
Wanasiasa hao ni Stephen Byabato aliyekuwa mbunge wa Bukoba Mjini mkoani Kagera na Cosato Chumi aliyekuwa mbunge wa Mafinga Mjini mkoani Iringa.
Wawili hao walishindwa kupenya katika hatua tofauti za uteuzi na kura za maoni za ndani ya CCM, hatua iliyowafanywa kushindwa kupata nafasi ya kutetea majimbo yao.
Sio hao tu, yumo Kambarage Wassira aliyewania ubunge wa Bunda, ambaye licha ya kuongoza kura za maoni, lakini hakufanikiwa kupenya badala yake Kamati Kuu ya CCM kurudisha jina Ester Bulaya aliyekuwa ameshika nafasi ya tatu.
Mbali na hao, kikao hicho kimewapitisha Chikulupi Kasaka, Fatuma Kange na Jesca Mshama, kwa upande wa wanawake kuwania nafasi ubunge wa Eala.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumatano Aprili 29,2026 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, wengine walioteuliwa ni Jabir Bwanika na Dk Suleiman Serera na Paschal Masalu.
Wagombea hao tisa wanawania nafasi tatu za ubunge wa Eala, zilizoachwa wazi na Angela Kizigha, Ng’waru Maghembe na James Ole Millya waliteuliwa na kuchaguliwa kuwa wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uteuzi wa wagombea hao utafanyika kesho Alhamisi Aprili 30 bungeni jijini Dodoma saa 10 jioni na Mei 4 saa tano asubuhi mchakato wa uchaguzi utafanyika baada ya kipindi cha maswali na majibu kumalizika.
Vunjabei abwagwa
Licha ya kuibuka kidedea katika mchakato wa kura za maoni uliofanyika Aprili 18, 2026 jina la Fred Ngajiro maarufu Vunjabei, limeshindwa kupenya katika kikao cha Kamati Kuu.
Katika mchakato wa kura za maoni Vunjabei aliongoza kwa kura 2,703, akifuatiwa na Festo Kiswaga (868), Emmanuela Mtatifikolo (662) na Arif Abri (233).
Kwa lugha nyingine, aliyekuwa mshindi wa tatu wa kura za maoni Mtatifikolo ndiye aliyepitishwa kuipeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi wa Isimani, baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, William Lukuvi kufariki dunia Machi 25, 2026.