Tanga. Manjozi na vilio vimetawala wakati wasanii, ndugu, jamaa na marafiki wakimpumzisha aliyekuwa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Suleiman Vunde maarufu Spack, kwenye nyumba yake ya milele katika makaburi ya Mwakidila jijini Tanga.
Mazishi hayo yalihudhuriwa na watu mbalimbali, huku wakikumbuka mchango wake kwenye muziki wa Bongo Fleva ulivyogusa maisha ya wengi.
Msanii wa kizazi kipya Tuna Man akishiriki kwenye mazishi ya Spark. Picha Mbonea Herman
Shangazi wa marehemu, ambaye pia alimtaja kuwa karibu sana naye, Rehema Domo amesema kifo cha Spack kimeacha pengo katika familia yao.
Amesema Spack enzi za uhai wake, amewahi kumweleza kuwa alikuwa anakumbana na changamoto, lakini hakuwahi kufafanua ni zipi hasa.
“Alikuwa akiniambia shangazi nina mitihani,’ lakini hakuwa ananiambia chochote zaidi ya hapo. Mwaka jana aliniambia hivyo na juzi alinipigia tena simu akirudia maneno yale yale… Sikujua kinachomsibu ni nini. Jana nikapata taarifa kuwa ndugu yako amefariki,” amesimulia.
Ameongeza kuwa familia ilipokea msiba huo kwa maumivu na kulikuwa na mjadala kuhusu mahali pa mazishi
“Kwa kweli roho imeniuma. Familia tulipokea msiba kwa uchungu. Ilikuwa inapendekezwa azikwe Dar es Salaam, lakini tukasema haiwezekani, lazima azikwe Tanga, palepale tulipozaliwa.”
Kwa upande wake, msanii wa muziki wa kizazi kipya, Khalid Ramadhan ‘Tunda Man’, amemuelezea Spack kama msanii mbunifu na mwenye mchango mkubwa katika kukuza vipaji vya vijana.
“Msiba huu siyo wa familia pekee, bali ni wa wasanii wote. Tulikutana kupitia marehemu Abdu Bonge baada ya kila mmoja kutoa ngoma yake ya kwanza. Tukafanya kazi pamoja na nyimbo zetu zilifika mbali na kuwahamasisha wasanii wengi chipukizi kuingia kwenye muziki.” Ameeleza Tunda Man.
Ameongeza kuwa ingawa hawakuwa wakifanya kazi pamoja kwa karibu kabla ya kifo chake, bado walikuwa na ukaribu.
Mwili wa msanii Spark ukishushwa kwenye gari katika makaburi ya Mwakidila jijni Tanga.Picha na Mbonea Herman
“Nilikuwa na shughuli nyingi na yeye zamani. Japo baadaye kila mmoja alikuwa kwenye njia yake, lakini familia yake ilikuwa kama familia yangu. Kifo chake kimeniumiza sana,” Ameeleza.
Tunda Man pia alikanusha baadhi ya madai kwamba huenda msongo wa mawazo umechangia kifo chake, akieleza kuwa msanii huyo alikuwa ameanza kurejea katika hali nzuri ya maisha.
“Ni kweli alipitia changamoto za kiuchumi, lakini baada ya muda mambo yalikuwa yanaenda vizuri. Alikuwa ameanza kuisimamia familia yake, watoto wake waliokuwa sehemu tofauti aliwakusanya pamoja, akalipia ada na kodi ya nyumba. Pia, alikuwa na mipango ya kufanya video ya kazi zake mpya,” amesema.
Promota wa muziki wa Bongo Fleva, Mbwana Imam ‘Arbab’, ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa marehemu tangu utotoni, amesimulia safari ya Spack kabla hajapata umaarufu.
“Tulikuwa wote Mtaa wa Mzingani, Tanga. Kuna siku alinifuata akaniambia ndoto zake za kufanya muziki. Kwa kweli sikumchukulia serious wakati ule, niliona kama utani tu.”
Amesema baadaye alishtuka kusikia wimbo maarufu walioufanya pamoja na Tunda Man:
“Baadaye nikasikia wimbo ‘Nipe Ripoti’ alioufanya na Tunda Man ulikuwa unatamba. Siku moja tulikuwa tukizindua kambi yetu Tanga, tukasema lazima tumtafute aje atuwakilishe. Alikuja na kufanya vizuri, tena bila hata kudai malipo kwa sababu ilikuwa ni kazi ya mtaani,” amesimulia.
Picha ya marehemu Spack enzi za uhai wake
Arbab aliongeza kuwa tangu wakati huo walipotezana kwa muda mrefu, na kifo chake kilimkuta bila kupata nafasi ya kuonana naye tena:
“Zaidi ya miaka 20 hatukuwahi kukutana tena. Kusikia amefariki imeniuma sana.”
Pia alionesha masikitiko yake kuhusu mwitikio mdogo wa baadhi ya wasanii kutoka Dar es Salaam katika mazishi hayo, akisisitiza kuwa mchango wa Spack ulipaswa kutambuliwa zaidi.
Wengi wanamkumbuka kama msanii mwenye kipaji, mpole na mwenye ndoto kubwa ambazo zimekatishwa ghafla.
Sheikh Omar Khalfan ambaye aliyeongoza swala ya mazishi, amewataka waombolezaji kuchukulia kifo hicho kama funzo la kuhimizana kuwatendea mema binadamu wengine, kwa kuwa hakuna anayejua ni lini atakutwa na mauti.
“Kifo cha Spack kila mmoja wetu hapa achukue funzo… tunaambiwa jioni alikuwa mzima wa afya lakini asubuhi akakutwa amefariki dunia,” amesema Sheikh Khalfan.